1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yanaendelea nchini Misri

13 Julai 2011

Maelfu ya wamisri walikusanyika mbele ya makao makuu ya serikali mjini Cairo,wakidai livunjwe baraza kuu la vikosi vya wanajeshi linaloitawala nchi hiyo tangu February 11 mwaka huu..

https://p.dw.com/p/11u6k
Waandamanaji katika uwanja wa Tahriri mjini CairoPicha: picture alliance / dpa

Hapo awali wanajeshi waliwaonya waandamanaji waliokusanyika katika uwanja wa Tahrir tangu ijumaa iliyopita,wakisema hatua zote za kisheria zitachukuliwa ili kurejesha utulivu katika mji mkuu Cairo.

Waandamanaji hao wanapaza sauti dhidi ya utawala wa kijeshi.Wanadai ajiuzulu mkuu wa baraza kuu la vikosi vya wanajeshi Marshal Mohamed Hussein Tantawi.Mbali na waandamanaji hao katika uwanja wa Tahrir,kitovu cha mapinduzi ya Nil,wengine walikusanyika pia kuanzia Suez hadi Alexandria.

Wamisri wengi wanalilaumu baraza kuu hilo kwa kushindwa kutekeleza ahadi walizotoa na kuchelewesha kesi dhidi ya viongozi wa utawala wa zamani wa Hosni Mubarak.

Ägypten Kairo Proteste Flash-Galerie
Waandamanaji wanabeba bango dhidi ya watawala wa kijeshiPicha: picture alliance/dpa

"Inakuwaje,Hosni Mubarak anatibiwa katika hospitali ya fahari kabisa na wale ambao wamejeruhiwa wakati wa mapinduzi wanapelekwa katika hospitali mbovu,na kuna hata wanaotolewa kwa nguvu katika hospitali hizo.Haieleweki.La,tunataka watu wote watendewe haki,hatukubali kusingiziwa eti tunayofanya si haki.Kila mtu ana haki ya kudai haki zake.Yeyote aliyeuwa au kuiba anabidi alipe maovu aliofanya."

Ahadi za waziri mkuu Essam Charaf za kuibadilisha serikali yake,zinaonyesha kutotuliza hasira za waandamanaji wanaodai mbali na kuharakishwa kesi dhidi ya watala wa zamani,wanataka pia mageuzi ya kidemokrasi.

Jana waziri mkuu amekubali kujiuzulu kwa makamo wake Yehia al Gamal ambae waandamanaji wanadai hana lake.

"Vikosi vya wanajeshi vinatambua dhamana zao za kihistortia na jukumu lao kwa taifa na tunawatolea mwito raia wasikubaliane na waandamanaji wanaopinga hali isirejee kuwa ya kawaida." amesema jenerali Mohsen Fangary wa baraza kuu la kijeshi katika tarifa yake hapo jana.

Tahrir Platz sit-in
Waandamanaji wameahidi kupiga kambi hadi madai yao yanaitikwaPicha: picture alliance / dpa

Uchaguzi wa bunge uliokuwa uitishwe September mwaka huu,umeakhirishwa hadi November.Uamuzi huo umepitishwa ili kujibu miito ya baadhi ya vyama vya kisiasa ili kuweza kujitayarisha vya kutosha.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters,/AFP

Mhariri:Abdul-Rahman