1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano yaendelea Misri

30 Januari 2011

Waandamanaji nchini Misri wamepuuza amri ya serikali ya kutotoka nje na wameendelea kukusanyika katika barabara za mji mkuu Cairo, huku wakitoa wito wa kujiuzulu rais wa nchi hiyo, Hosni Mubarak.

https://p.dw.com/p/107Ip
Kiasi ya watu 100 wanasemekana kufariki tangu kuanza maandamano nchini Misri.Picha: picture-alliance/dpa

Inatathminiwa kuwa kiasi ya waandamanaji elfu 50 walikusanyika katika Uwanja wa Tahrir katikati ya Cairo, huku maandamano yakifanyika pia katika miji ya Alexandria na Suez.

Ägypten Kairo Proteste
Kiongozi wa upinzani Mohamed El Baradei:Picha: picture-alliance/dpa

Mohamed El Baradei,anaeongoza kampeni ya upinzani, aliwahotubia waandamanaji na katika hotuba hiyo alitoa wito kwa Rais Mubarak kuondoka Misri upesi iwezekanavyo. El Baradei akaongezea kuwa uteuzi wa hapo jana, wa makamu mpya wa rais na waziri mkuu, hautotosha kumaliza machafuko ya siku tano dhidi ya rais Mubarak na serikali yake. Mapema hapo jana baraza zima la mawaziri liliwasilisha barua za kujiuzulu. Hadi sasa, kiasi ya watu 100 wameuwawa katika mapigano yaliyozuka kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama.

Jumuiya ya kimataifa imewaomba maafisa wa serikali nchini Misri, kuzuia mapambano na waandamanaji. Katika taarifa ya pamoja,Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron na Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy wamemuhimiza Rais Hosni Mubarak wa Misri kuzuia matumizi ya nguvu. Vile vile wamesema kuwa haki za binadamu na uhuru wa kidemokrasia unapaswa kuheshimiwa kikamilifu.

Weltwirtschaftsforum Davos Bundeskanzlerin Angela Merkel
Picha: AP

Viongozi hao watatu, wametoa mwito kwa rais huyo wa Misri aliekumbwa na machafuko, kuwajibika kufanya mageuzi kuitikia kile walichokiita "malalamiko halali" ya wananchi wake. Wakati huo huo, Marekani hapo jana ilisema kuwa haitoshi tu kupanga upya baraza la mawaziri. Ilitamka hayo baada ya Mubarak kuivunja serikali yake na kudhihirisha kuwa yeye hana azma ya kuondoka madarakani. Rais Barack Obama wa Marekani alisema kinachohitajika ni hatua thabiti zinazoendeleza haki za umma wa Misri, majadiliano ya maana kati ya serikali na wananchi wake, na mwelekeo wa mageuzi ya kisiasa yatakayoleta mustakabali ulio na uhuru mkubwa, fursa zaidi na haki kwa watu wa Misri.

Mwandishi Maryam Abdalla/Rtre
Mhariri:Prema Martin.