Maandamano yachacha Iran
18 Juni 2009Vyombo vya habari vya serikali vilitangaza kuwa watu saba waliuawa wakati wa maandamano ya Jumatatu ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika wiki iliyopita.Moussavi na wafuasi wake wanashikilia kuwa matokeo hayo ya uchaguzi yana dosari.
Rais Mahmoud Ahmedinejad ametangazwa mshindi rasmi wa uchaguzi huo.Maandamano yamekuwa yakiendelea kwa siku tano mfululizo.Uongozi wa Iran kwa upande wake unasisitiza kuwa matokeo ya uchaguzi ni sahihi na kwamba serikali za mataifa ya magharibi zinaingilia mambo ya ndani ya nchi yao.
Wakati huohuo Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imetangaza kuwa huenda uchaguzi wa rais wa Iran umegubikwa na utata.Kauli hiyo imetolewa na msemaji wa Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani Ulrich Wilhelm.Wabunge wa Ujerumani walilijadili suala hilo na hali nzima ya Iran na wanawaunga mkono waandamanaji wanaoyapinga matokeo.Kwa sasa wito umetolewa kwa uongozi wa Iran kuwaachia huru waandamanaji wanaozuiliwa,uchunguzi wa vifo vilivyotokea kufanywa pamoja na kuwaruhusu waandishi wa habari kuutangaza mvutano wenyewe uliopo.