1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya upinzani nchini Kenya yaingia siku ya tatu hii leo

18 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CuI0

Maandamano ya upinzani nchini Kenya kupinga ushindi wa rais Mwai Kibaki katika uchaguzi uliopita, yameingia siku yake ya tatu hii leo.

Hatua ya serikali kuyapiga marufuku maandamano yote haikufaulu katika siku mbili zilizopita huku maandamano yakifanywa katika miji mbalimbali nchini humo.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amesema amilaumu serikali na polisi kwa kuwaua waandamanaji wasio na hatia.

Ulinzi umeimarishwa katika bustani ya Uhuru Park mjini Nairobi, mahala ambapo mkutano mkubwa wa hadhara wa upinzani umepangwa kufanyika hii leo.

Msemaji wa chama kikuu cha upinzani nchini Kenya Orange Democratic Movevement, amesema baada ya mkutano wa leo maandamano yatamalizika rasmi.

Upinzani unapania kuwashawishi wafuasi wake kuzigomea biashara zinazomilikiwa na mawaziri serikalini na kuzivamia kampuni kadhaa.

Chama cha ODM kimesema kitashirikiana na katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, Bi Graca Machel, mke wa rais wa zamani wa Afrika Kusini, na rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa, ambao wote wawili waliwasili jana mjini Nairobi.

Bwana Kofi Annan bado anasubiriwa mjini humo.