Maandamano nchini Ufaransa kuendelea
22 Oktoba 2010Paris.
Vyama sita vikuu vya wafanyakazi nchini Ufaransa vimetoa wito kwa wapinzani wa mageuzi ya mpango wa pensheni kufanya maandamano makubwa kwa muda wa siku mbili zaidi katika wiki zinazokuja licha ya kura ya mwisho kutarajiwa kupigwa na baraza la Seneti leo Ijumaa. Rais Nicolas Sarkozy , ambaye anataka kiwango cha chini cha umri wa kustaafu kiongezwe kutoka miaka 60 hadi 62 ili kupunguza gharama , amevishutumu vyama vya wafanyakazi kwa kuvuruga hatua za kufufua uchumi dhaifu wa ufaransa. Jana Alhamis polisi wa kuzuwia ghasia walipambana na vijana mjini Lyon na Poitiers wakati wafanyakazi waliogoma wakiendelea kuweka vizuwizi katika viwanda 12 vya kusafishia mafuta na robo ya vituo vya kuuzia mafuta nchini humo havina mafuta. Ni nusu tu ya treni ziendazo mikoani zimekuwa zikifanyakazi. Vyama vya wafanyakazi , ikiwa ni pamoja na chama chenye nguvu cha CGT, vimepanga maandamano Alhamis ijayo na Novemba 6. Hatua za kushughulikia maandano hayo zinazochukuliwa na rais Sarkozy zinaangaliwa kwa karibu na serikali nyingine za umoja wa Ulaya ambazo nazo zinapanga hatua za kubana matumizi.
Mwandishi : Sekione Kitojo / RTRE