Maandalizi ya michezo ya Olimpik yaendelea | Michezo | DW | 07.08.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Maandalizi ya michezo ya Olimpik yaendelea

Mwaka mmoja umesalia kabla michezo ya Olimpik kuanza nchini China

Wanafunzi wa vyuo vikuu vya China wakionyesha mazoezi ya Tai Chi mjini Quandai

Wanafunzi wa vyuo vikuu vya China wakionyesha mazoezi ya Tai Chi mjini Quandai

Miaka sita tangu mji wa Beijing uliposhinda nafasi ya kuandaa michezo ya Olimpiki mwaka wa 2008, utawala wa China umejitolea kwa dhati kutumia michezo hiyo kuondoa sifa mbaya. Unataka kuonyesha ukarimu wake na kudhihirisha imepiga hatua katika teknolojia ya kisasa. Licha ya gharama kubwa, fedha zitatumika bila wasiwasi wa bajeti na bidii ya wafanyakazi haitafifia.

´Tuko tayari´ ni maneno yaliyojumulishwa kwenye wimbo ulioimbwa na waimbaji wawili kutoka Hongkong. Jumamosi ya mwisho kabla kuanza michezo ya Olimpik mjini Beijing, wimbo huo utazinduliwa kama muziki utakaotangulia nyimbo nyengine 30 zitakazoimbwa Jumamosi ya tarehe 8 mwezi Agosti mwaka ujao.

Kazi ya ujenzi inayofanywa na Wachina ni ya kuridhisha. Maeneo 12 kati ya 39 ya mashidano yatakarabatiwa upya. Tayari uwanja wa Olympia uliojengwa mfano wa kiota cha ndege umekuwa kivutio cha usanifu. Miundombinu ya Peking itafanyiwa ukarabati mkubwa. Euro milioni 400 zitatumiwa kujenga reli mbili mpya.

Serikali ya kikomunisti ya China imejitolea kwa dhati kuhakikisha mashidano ya Olimpik ya mwaka ujao yanafaulu na matatizo yote yatakayotokea yatatatuliwa barabara. Pia katika vitongoji vya mji wa Beijing watu takriban milioni moja unusu watalazimika kuhamishwa kufikia mwezi Agosti mwaka ujao, wengi wao kwa kulazimishwa. Hayo yamesemwa na taasisi inayohusika na haki ya makaazi na kuwahamisha watu kwa nguvu, COHRE, mjini Geneva Uswisi.

Mji wa Beijing umebadilika na uchumi umeendelea kushamiri. Hein Verbruggen, mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya michezo ya Olimpik, IOC, alisema baada ya ziara yake mjini Beijing kwamba anaridhika jinsi maandalizi yanavyoendelea.

´Wako katika kasi nzuri ya maandalizi ambayo tungetarajia. Kila wakati tunapokuja tunazidi kufurahishwa tunapoyatembelea maeneo kutakakofanyika mashindano. Na nalazimika kusema ni mhemuko wakati unapofikiria kwamba utaweza kushiriki kwenye mashindano kwenye mazingira haya mazuri na ya kuvutia. Na nadhani nyote mnakubaliana nami kuwa ni jambo linalostahili kuzungumziwa.´

Ikiwa kasi ya mandalizi itaendelea kama ilivyo hivi sasa, viwanja vyote na kumbi za mashindano zitakamilika kufikia mwishoni mwaka huu. Mwisho kabisa ni kumalizika kwa kazi ya ujenzi wa uwanja unaojengwa mfano wa kiota cha ndege mnamo mwezi Machi mwaka ujao.

Naibu kiongozi wa kamati ya maandalizi mjini Beijing, Wang Wie, amesema, ´Tunaendelea vizuri kabisa na kazi ya maandalizi ya mashindano ya Olimpik kama ilivyopangwa.´

Ukosoaji kuhusu upungufu wa chakula au hali ya mazingira ni maswala yaliyopuuzwa na kamati ya maandalizi, lakini jambo linaloitia wasiwasi kamati hiyo ni kwamba Wachina wenyewe wanaweza kuiabisha serikali mbele ya wageni. Jiang Xiaoyu, pia ni naibu katika kamati ya maandalizi..

´Changamoto mojawapo kwetu ni vipi tutakavyoweza kuboresha programu za kompyuta na viwango vya utoaji wa huduma wakati wa michezo ya Olimpik. Hiyo ina maana kuboresha huduma, kuboresha mazingira na utamaduni wa maisha ya mji, vile vile kuongeza ubora wa utamaduni wa wakaazi.´

Ndio maana wakaazi wa Beijing watashuhudia kampeni kadhaa za kushangaza. Kutema mate kumepigwa marufuku na anayefanya hivyo atakamatwa na kushtakiwa. Watu wanalazimika kufanya mazoezi ya foleni ndefu na wanahimizwa wajifunze kiingereza. Quan You ni mkaazi wa mji wa Beijing.

´Hata wazee wenyewe wakiwa na umri wa miaka 70 huanza kufikiri; Aaah nalazimika kujifunza lugha ya kiingereza. Naiona lugha hiyo kuwa maalumu. Mashindano ya Olimpik sio swala la Marekani au Uingereza, bali ulimwengu mzima. Pia wanariadha kutoka nchi zisizozungumza kiingereza hawawezi kujifunza kiingereza kila siku. Haya ni mashindano ya michezo na wala sio mashindano ya lugha.´

Idadi kubwa ya Wachina wanataka kushiriki katika maandalizi ya michezo ya Olimpik. Watu laki moja walitakiwa wajitolee kusaidia kazi ya maandalizi, lakini watu zaidi ya nusu milioni wakawasilisha majina yao.

 • Tarehe 07.08.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHbR
 • Tarehe 07.08.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHbR