1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandalizi ya dimba la Kombe la Afrika yaendelea

2 Januari 2017

Gabon inajiandaa kuzikaribisha timu zitakazoshiriki katika dimba kubwa la kandanda barani Afrika, Kombe la Mataifa ya Afrika – AFCON litakalong'oa nanga Januari 14

https://p.dw.com/p/2V9lF
Issa Hayatou
Picha: picture-alliance/AP Photo/Ammar

Na mojawapo ya timu zitakazotua Gabon ni Uganda Cranes, ambayo ndiye mwakilishi pekee wa kanda ya Afrika Mashariki. Baada ya uvumi kusambaa kuwa timu hiyo haingeweza kucheza michuano yake ya  kirafiki kutokana na ukosefu wa fedha, vijana hao walitua jana nchini Tunisia. Cranes wanatarajiwa kucheza mechi za kuyanoa makali dhidi ya Tunisia, Slovakia na Cote d'Ivoire kabla ya kusafiri kwenda Gabon.

Kwa sasa timu mbalimbali zinaendelea kuvitaja vikosi vyao vitakavyotua Gabon, na kuna baadhi ya majina au wachezaji nyota ambao mashabiki wa kandanda hawatakuwa na fursa kuwaona katika dimba hilo kutokana na sababu moja au nyingine…. Wachezaji Sofiane Feghouli wa Algeria na Hakim Ziyech wa Morocco na Bassem Morsy wa Misri ni miongoni mwa majina yatakayokosekana katika dimba hilo. Wote hawakupewa nafasi na makocha wao

Mshambuliaji wa Bournemouth ya England, Benik Afobe, ameamua kujiondoa katika AFCON ili kubakia na timu yake ya Premier League. Hayo ni licha ya yeye kuamua kuitelekeza timu ya taifa ya Uingereza na kutangaza kuwa mchezaji wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Vyombo vya habari vya Uingereza vimeripoti kuwa Afobe alimwambia kocha wa timu ya Congo Florent Ibenge kuwa angetaka kubaki Uingereza na kuiimarisha nafasi yake katika kikosi cha kwanza cha Bournemouth baada ya kufunga bao dhidi ya Swansea City katika ushindi wao wa 3-0 siku ya Jumamosi. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ina kundi gumu ambapo itapambana na mabingwa watetezi Cote d'Ivoire, Morocco na Togo katika Kundi C.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Iddi Ssessanga