Maambukizi ya homa ya nguruwe yabadilika
30 Aprili 2009Onyo hilo lina maana kuwa ugonjwa huo unaweza kusambazwa kati ya binadamu vilevile kati ya mataifa mawili kwa uchache.Hilo limesisitizwa na Mkuu wa Usalama wa Afya wa Shirika la Afya Ulimwenguni WHO Keiji Fukuda aliyesema kuwa ''Kwa sasa hakuna ushahidi wowote unaonyesha kuwa virusi hivi vinasambaa kutoka kwa nguruwe hadi binadamu.Virusi hivi vinaonekana kuwa vinasambaa kutoka mtu mmoja hadi mwengine.''
Kwa sasa mataifa hayo mawili ni Marekani na Mexico ambako ndiko chanzo cha virusi hivyo.
Kwa mujibu wa taarifa mtu mmoja amethibitishwa kuwa amefariki kwasababu ya homa hiyo nchini Marekani na wengine 91 wameambukizwa.Vifo 159 vya kwanza vimeripotiwa kutokea nchini Mexico na watu wengine 2500 tayari wameambukizwa virusi hivyo nchini humo.Kwa sasa watu wengine kadhaa wameripotiwa kuambukizwa virusi vya homa ya nguruwe katika mataifa mengine 26 kote ulimwenguni.
Katika bara la Ulaya visa vipya vya maambukizi vimeripotiwa na kuthibitishwa katika nchi za Ujerumani na Austria.Mpaka sasa watu watatu wameambukizwa virusi hivyo hapa Ujerumani,mmoja huko Austria,watano Uingereza na wengine 10 Uhispania.Mataifa mengine barani Ulaya yako chonjo na yanachukua tahadhari zinazohitajika.
Mwandishi:Thelma Mwadzaya /RTRE