1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa wa polisi wawashambulia waandamanaji Myanmar

Amina Mjahid
15 Februari 2021

Maafisa wa usalama wamewafyatulia risasi waandamanaji waliokuwa wakiandamana katika mji wa Mandalay nchini Myanmar wanaotaka kiongozi aliyepinduliwa Aung San Suu Kyi aachiliwe huru.

https://p.dw.com/p/3pOEg
Myanmar | Proteste nach Militärputsch
Picha: AP/dpa/picture alliance

Kulingana na Taarifa za vyombo vya habari, vilivyomnukuu mwaandishi habari mmoja nchini humo, polisi na wanajeshi walifyatua risasi kiholela majumbani mwa watu, na picha zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zinaonesha watu wakiwa wamejeruhiwa kwa kile kinachosemekana kuwa majeraha yanayotokana na risasi za mpira.

Hadi sasa haijawa wazi iwapo maafisa hao wa usalama walitumia risasi za moto na iwapo kuna waliokufa katika makabiliano hayo.

Mikanda mingine ya video iliwaonyesha maafisa wa polisi wakitembea barabarani na virungu. Watu kadhaa wanasemekana kukamatwa.

soma zaidi: Suu Kyi kuendelea kuzuiliwa wakati maandamano yakiendelea

Waandamanaji nchini Myanmar wamekuwa wakiandamana kwa siku 10 mfululizo wakitaka utawala wa kiraia urejeshwe chini ya kiongozi wa taifa hilo aliyepinduliwa Aung San Suu Kyi, huku wakishinikiza kuachiwa kwake baada ya jeshi kuipindua serikali na kumkamata kiongozi huyo wa chama cha NLD.

Vile vile kumeripotiwa makabiliano mengine kati ya polisi na waandamanaji mjini Yangon ambako waandamanaji walishambuliwa na wanajeshi kadhaa na mawasiliano ya Intaneti kukatwa usiku kucha.

Umoja wa Mataifa waitolea mwito Myanmar kuzingatia amani

 Myanmar  Regierungschefin Aung San Suu Kyi Putsch
Kiongozi wa Myanmar aliyepinduliwa madarakani Aung San Suu Kyi Picha: Lynn Bo Bo/dpa/picture-alliance

Huku hayo yakiarifiwa Katibu Mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres, kupitia msemaji wake Stephane Dujarric, amesema anawasiwasi wa kamata kamata inayoendelea kwa viongozi wa kisiasa, maafisa wa serikali, maafisa wa mashirikia ya kiraia na wawakilishi wa vyombo vya habari pamoja na kukatwa kwa mawasiliano ya intaneti. Guterres amesema haya yote hayapaswi kufanyika ili kuhakikisha uhuru wa kujieleza unaojumuisha haki ya kupata habari.

Wakati huo huo kesi inayomkabili Kiongozi Aung San Suu Kyi iliyopaswa kusikilizwa hii leo mahakamani imeahirishwa hadi siku ya Jumatano, hii ikiwa ni kulingana na gazeti moja nchini humo.

soma zaidi: Umoja wa Mataifa watakiwa kuweka vikwazo Myanmar

Suu Kyi anatuhumiwa kwa makosa ya kukiuka sheria za biashara za kigeni kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliofanyika Februari Mosi. Kyi aliye na miaka 75 analazimika kubakia kizuizini hadi kesi yake itakaposikilizwa na haijawa wazi iwapo atakuwepo mahakamani yeye mwenyewe au ataunganishwa kupitia kiungo cha vidio

Mapinduzi ya kijeshi nchini humo yalifanyika baada ya uchaguzi wa Novemba uliokipa chama cha Suu Kyi cha NLD ushindi mkubwa ingawa jeshi limesema kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu bila ya kutoa ushahidi wowote. Jeshi limeweka hali ya dharura ya mwaka mmoja  na kuweka kile wanachokisema ni serikali ya muda kabla ya uchaguzi mpya kuandaliwa.

Suu Kyi bado hajaonekana kwa wiki mbilina juhudi za Marekani za kuwasiliana nae zimekataliwa na jeshi. Wakili wake pia amenyimwa nafasi ya kuwasiliana nae moja kwa moja.

Chanzo: dpa