Maabara ya Curiosity yatua salama Mars | Masuala ya Jamii | DW | 06.08.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Maabara ya Curiosity yatua salama Mars

Chombo cha maabara ya sayansi ya sayari ya Mars kinachomilikiwa na shirika la anga la Marekani NASA, kilichopewa jina la Curiosity, kimefanikiwa kuwasili katika Sayari Nyekundu ya Mars siku ya Jumapili jioni.

Chombo cha shirika la NASA cha Curiosity.

Chombo cha shirika la NASA cha Curiosity.

Waongozaji wa chombo hicho waliripuka kwa furaha pale walipopokea ishara kuthibitisha kuwa chombo hicho kimevuka vizingiti na kimewasili salama katika shabaha yake, mwishoni kabisa mwa shimo pana la kale lililoko katika sayari hiyo. Chombo hicho cha maabara kilisafiri kwa zaidi ya miezi minane, kwa umbali wa kilomita 566 milioni, sawa na maili milioni 352 kabla ya kuchana anga la Mars kwa mwendo wa maili 13,000 kwa saa, ambao ni mara 17 zaidi ya mwendo wa sauti, na baadaye kikaanza kushuka.

Wajumbe wa timu iliyoratibu safari ya Curiosity wakishangalia baada ya kupata ishara ya kutua salama kwa chombo hicho katika sayari Nyekundu ya Mars.

Wajumbe wa timu iliyoratibu safari ya Curiosity wakishangalia baada ya kupata ishara ya kutua salama kwa chombo hicho katika sayari Nyekundu ya Mars.

Muda mchache baada ya kushuka, Curiosity ilituma picha tatu za kwanza kutoka katika uso wa sayari ya Mars, moja wapo ikionyesha tairi la gari na kivuli cha chombo hicho kilivyoonekana kwenye ardhi hiyo yenye miamba. "Siwezi kuamini, haya ni maajabu," alisema Allen Chen, ambaye ni naibu kiongozi wa timu iliyoratibu safari ya chombo hicho iliyo na makao yake katika maabara ya vyombo vinavyoendeshwa kwa injini za jeti karibu na mji wa Los Angeles.

Kushuka kwa chomo hiki katika anga nyembamba ya Mars, ambacho ni kitendo kinachochukuliwa kuwa cha maajabu na mafanikio ya hatari zaidi katika safari za anga za roboti, kulichukua muda mchache sana, jambo ambalo lilikuwa la afueni kwa shirika la NASA.

Kushuka kwa Curiosity

Curiosity, ambayo ilikuwa imefungwa kwenye roketi yenye sura ya kapsuli, ilitumia mfumo wake wa kipekee wa kujiendesha yenyewe kupunguza mwendo wake kabla ya kutua. Baadaye ilifungua mwavuli mkubwa na winchi ya angani ambayo haijawahi kutumiwa, kutua ndani ya bonde kubwa linaloitwa Gale Crater, lililoko karibu na mstari wa katikati wa Equator wa sayri hiyo katika kizio cha kusini cha dunia.

Wakati wa kutua kwa Curiosity vyombo viwili vya NASA na cha tatu kinachoendeshwa na shirika la anga la Ulaya vilikuwa vinakatiza juu kwa ajili ya kurejesha taarifa duniani. Akizungumzia mafanikio ya chombo hicho, Mkurugenzi katika kituo cha anga cha Umoja wa Ulaya, Rider Thomas alisema:

"Tunatarajia sasa tutapata uvumbuzi adhimu wa kisayansi. Lengo ni kupata ushahidi kuwa kulikuwepo na maisha au maisha bado yapo katika sayari ya Mars. Na pengine baada ya miongo miwili au mitatu, wanadamu wanaweza kwenda kuishi katika sayari."

Moja ya picha zilizotumwa na Curiosity baada ya kuwasili katika sayari nyekundu ya Mars.

Moja ya picha zilizotumwa na Curiosity baada ya kuwasili katika sayari nyekundu ya Mars.

Chombo hicho kinakusudiwa kukusanya taarifa zitakazowezesha kujua kama sayari hiyo inavyo, au iliwahi kuwa na viambato muhimu vya maisha.

Maabara ya sayari ya Mars ambayo imegharimu dola za Marekani bilioni 2.5 ndiyo mradi wa kwanza wa shirika la NASA wa astro-bayolojia, yaani elimu ya viumbe katika anga za juu, kwenda katika sayari hiyo tangu ile ya Viking ya miaka ya 1970. Mradi huo umesanifiwa kudumu kwa mwaka moja wa sayari ya Mars, ambao ni sawa na siku 687 za hapa duniani.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\RTRE
Mhariri: Othman Miraji

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com