1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON : Uingereza yajaribu kudhibiti gonjwa la mifugo

5 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBc1

Uingereza inajaribu kudhibiti mripuko wa ugonjwa wa miguu na midomo wenye maambukizi makubwa kwa kuwachinja n’gombe kwenye shamba moja nje ya London ili kuzuwiya marudio ya hasara kubwa iliosababishwa na mripuko wa gonjwa hilo miaka sita iliopita.

Wizara ya Mazingira imesema kirusi kilichopatikana kwenye n’gombe walioambukizwa katika mji wa Surrey kusini magharibi mwa London sio kile kilichonekana karibuni kwenye wanyama.

Ikiwa ni matokeo ya mripuko wa gonjwa hilo kwenye shamba moja Uingereza imeamuwa kwa hiari kupiga marufuku usafirishaji nje wa mifugo na bidhaa za wanyama.

Mganga mkuu wa wanyama nchini Uingereza Debby Reynolds amezungumza na waandishi wa habari juu ya tahadhari inayochukuliwa na serikali.

Amesema hatua za haraka zimechukuliwa kuanzisha kanda ya hifadhi na uchunguzi.Na ziada ya hilo usafirishaji wa n’gombe, kondoo na nguruwe pamoja na wanyama wanaoweza kuathirika kwa urahisi umepigwa marufuku kabisa nchini kote Uingereza.

Hofu ya gonjwa hilo pia imepelekea Umoja wa Ulaya kupiga marufuku uagizaji wa mifugo kutoka Uingereza.

Janga la ugonjwa huo wa miguu na midomo hapo mwaka 2001 limepelekea kuchinjwa kwa mifugo milioni 7 pamoja na kuathiri vibaya sana sekta za kilimo na utalii.