1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LONDON : Ofisi ya Blair yashutumu utaratibu wa kumnyonga Saddam

7 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCcV

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair leo hii imesema waziri mkuu huyo alikuwa anaamini kwamba kulikuwa na makosa moja kwa moja kwa namna kiongozi wa zamani wa Iraq Saddam Hussein alivyonyongwa na hiyo kuongezea shutuma zilizotolewa na mawaziri wake waandamizi akiwemo Gordon Brown anayetazamiwa kuchukuwa nafasi ya Blair wakati atakapon’gatuka.

Ofisi yake imesema Blair anatazamiwa kuzungumzia hadharani kunyongwa kwa Saddam wiki hii lakini anaamini kwamba utaratibu uliotumika ulikuwa umesimamiwa vibaya.

Waziri wa Fedha Gordon Brown amesema hapo jana kwamba kukejeliwa kwa Saddam wakati wa kunyongwa kwake na kutolewa kwa kanda ya video ya kunyongwa huko iliorekodiwa kinyume na sheria ni jambo la kulaaniwa na lisilokubalika.

Waziri Mkuu wa Iraq Nouri al-Maliki ameamuru kufanyika uchunguzi juu ya kutolewa kwa ukanda huo wa video.

Waziri Mkuu wa Uingereza amesema anaunga mkono moja kwa moja uchunguzi huo lakini kuamini kwamba kulikuwa na makosa moja kwa moja juu ya jinsi Saddam alivyongwa lakini hakupaswi kuwafanya wasahao uhalifu uliotendwa na Saddam ikiwa ni pamoja na mauaji ya mamia kwa maelfu ya raia wa Iraq.

Blair amekuwa akikabiliwa na shinikizo ashirikiane maoni na mawaziri wake waandamizi juu ya kunyongwa kwa Saddam baada ya Naibu Waziri Mkuu John Prescott na Waziri wa Fedha Gordon Brown kushutumu utaratibu uliotumika kumyonga kiongozi huyo wa zamani wa Iraq.