Liverpool yaadhibiwa Manchester United hoi
23 Oktoba 2017Manchester United haikucheza na mtiririko wake wa kawaida kama ilivyo kwa mahasimu wake katika Premier League Manchester City ama Tottenham , mchezaji wa kati wa Huddersfield Town Tom Ince amesema baada ya ushindi wa mabao 2-1 wa timu yake dhidi ya kikosi cha kocha nyota Jose Mourinho siku ya Jumamosi.
Huddersfield iliangusha mbuyu siku ya Jumamosi ikiwa ni kipigo cha kwanza kwa kikosi cha Jose Mourinho msimu huu, ambapo mchezaji huyo wa kiungo , baba yake Paul Ince aliichezea Manchester United mara 204 katika miaka ya 90.
Nae kocha nyota Jurgen Klopp wa Liverpool aliona rangi zote kwa wakati mmoja jana Jumapili baada ya kikosi chake kuadhibiwa vikali na Tottenham Hot Spurs kwa mabao 4-1 na kushuhudia kipigo cha juu kabisa katika ligi hiyo yenye ushindani mkubwa barani Ulaya. Liverpool ambayo imeporomoka hadi nafasi ya tisa ikiwa na pointi 13 , imefungwa mabao 16 hadi sasa ikiwa ni udhaifu mkubwa wa safu ya ulinzi ambao kocha huyo anatakiwa kufanyia kazi.
Liverpool kukwaana na Huddersfield
Hata hivyo Liverpool itataka kurejea katika njia ya ushindi Jumamosi ijayo itakapokwaana na Huddersfield Town , inayoongozwa na kocha ambaye alikuwa pamoja nae katika benchi la ufundi la timu ya Borussia Dortmund, David Wagner.
Nchini Ufaransa , Neymar alikuwa shujaa na pia aliyetia doa wakati mshambuliaji huyo raia wa Brazil alipofunga bao na kisha kutolewa nje kwa kadi nyekundu wakati Paris Saint Germain ilipopata sare ya mabao 2-2 katika pambano kali la mahasimu wakubwa dhidi ya marseille katika League 1 jana Jumapili.
Baada ya Florian Thauvin kuifungia Marseille bao la pili , na Neymar akiwa na kadi ya njano moja tayari alionekana kupiga kichwa mshambuliaji wa marseille kutoka Argentina Lucas Ocampos na kutolewa kwa kadi ya pili ya njano.
Nchini Italia Sami Khedira wa Ujerumani alipachika mabao matatu katika ushindi wa mabao 6-2 ya Juventus Turin dhidi ya Udinese na kuweka mbio za kuwania ubingwa hai ikiwa Juventus inafukuzana na viongozi Napoli na Inter Milan.
Cristiano Ronaldo anaonekana kuwa mchezaji anayeweza kutoroka na taji la mchezaji bora wa FIFA katika mwaka 2017 kutokana na hali bora ya timu yake ya Real Madrid, sherehe zitakazofanyika mjini London leo Jumatatu.
Al Ahly yaingia fainali
Katika bara la Afrika Al Ahly ya Misri inakuwa klabu ya kwanza kupachika mabao 6 katika mchezo wa Champions League barani Afrika katika nusu fainali wakati walipowararua Etiole sahel ya Tunisia kwa mabao 6-2 mjini Alexandria jana Jumapili na kufikia fainali. Mabingwa hao mara nane wa taji hilo ilifuzu kwa jumla ya mabao 7-4 na kukabiliana na Wydad Casablanca ya Morocco katika fainali itakayochezwa kwa mikondo miwili ikiwa mkondo wa kwanza utafanyika mwishoni mwa juma nchini Misri.
Nayo TP Mazembe mabingwa watetezi wa kombe la CAF la Shirikisho wataoneshana kazi katika fainali na SuperSport ya Afrika kusini baada ya timu hizo kufuzu kuingia katika fainali itakayofanyika Novemba 19. Nchini Tanzania homa ya pambano la watani wa jadi Simba na Yanga hapo tarehe 28 mwezi huu imeanza kupanda na mashabiki wanalizungumzia pambano hilo kana kwamba linafanyika kesho.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe / dpae
Mhariri: Mohammed Abdul rahman