1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ligi ya Ujerumani kurejea dimbani wiki ijayo

Sekione Kitojo13 Januari 2012

ligi ya Ujerumani Bundesliga kurejea dimbani Ijumaa ijayo, timu zinarejea sasa kutoka katika matayarisho ya mzunguko wa pili.Vijana wadogo wawili wafungishwa mkataba kuzichezea timu za daraja la kwanza.

https://p.dw.com/p/13jVn
Ni pambano kati ya mabingwa Borussia Dortmund na FC Kolon katika bundesliga msimu huu.Picha: picture-alliance/dpa

Bundesliga kuanza Ijumaa

Hapa Ujerumani wakati timu za ligi daraja la kwanza , Bundesliga, zinarejea nchini kutoka mafichoni ambako zimekuwa zikipata mafunzo ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi hiyo , hatua ya timu mbili za daraja la kwanza kuwafungisha mkataba vijana wadogo wawili wenye umri wa miaka 13 imezua utata miongoni mwa wadau.

Vijana hao ambao wamefungishwa mkataba na timu za TSG Hoffenheim na VFL Wolfsburg wanatokea katika miji ya Berlin na Hamburg, na wataishi katika miji ambayo vilabu hivyo vinapatikana ikiwa ni kilometa nyingi kutoka nyumbani kwao , huku wakiungwa mkono na wazazi wao.

Hatua hiyo imezusha malalamiko kutoka kwa wadau wakitaka kukomeshwa kwa hatua hiyo ya kuwapora watoto.

Ilibidi kukubali uhamisho huo, lakini kwa mtazamo wangu kijana huyo hataweza kutoa uwezo wake wa asilimia 100 kwa Wolfsburg, amesema mkurugenzi wa vijana, Joachim Philipkowski, kuhusiana na kuondoka kwa kijana huyo kutoka timu hiyo. Ameondolewa kutoka katika mazingira ya familia yake. Na sifikiri kuwa hili ni jambo zuri.

Timu nyingine kadha pamoja na shirikisho la ligi ya Ujerumani , DFL, ambayo inaendesha ligi ya madaraja ya juu , pamoja na shirikisho la kandanda nchini Ujerumani, DFB, yameeleza wasi wasi wao.

Kulikuwa na makubaliano ya kiungwana hapo zamani kwamba haruhusiwi mtu kunyakua vipaji, amesema mkurugenzi mtendaji wa DFL , Holger Hieronymus. Kwa hiyo ameongeza kuna haja ya kuwa na makubaliano kama hayo tena.

VFB Stuttgart na Hannover 96 zimepinga vikali hatua hiyo .Hoffenheim na Wolfsburg wametetea uamuzi wao huo , zikisema uhamisho wa aina hiyo ni wa kawaida kabisa katika ligi nyingine zozote hapa Ulaya.

Wakati huo huo ligi ya daraja la kwanza nchini Ujerumani itarejea uwanjani siku ya Ijumaa wiki ijayo , ambapo Bayern Munich itakwaana na Borussia Moenchengladbach. Timu za Ujerumani zilifunga kambi katika nchi mbali mbali hapa Ulaya na hata mashariki ya kati, ambapo Bayern Munich ilikuwa nchini Qatar pamoja na Schalke 04 na Wolfsburg.

Bayern Munich pia ilitembelea nchini India na kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya taifa ya India , ambapo Bayern bila ya kupata upinzani wa kutosha , iliisambaratisha India kwa mabao 4-0.

Akizungumzia kuhusu matayarisho hayo kwa timu yake kocha wa Bayern Munich, Jupp Heynckes, amesema kuwa yalikuwa magumu na yalihitaji uvumilivu mkubwa kutoka kwa wachezaji wake.

"Ni dhahiri kuwa kulikuwa na hali ya mbinyo, kwasababu wachezaji walihitajika kufanya mazoezi mara mbili kwa siku. Na wamecheza mechi nne katika muda wa siku 12".

Wachezaji wa ligi ya Ujerumani , bundesliga, wamemchagua mchezaji wa kiungo wa Borussia Moenchengladbach, Marco Reus, kuwa mchezaji bora wa msimu hadi sasa.

Zaidi ya mchezaji mmoja kati ya watatu kati ya wachezaji 228 ambao walishiriki katika uchunguzi huo, walimchagua mchezaji huyo wa kimataifa wa ujerumani mwenye umri wa miaka 22 ambaye atahamia katika klabu ya Borussia Dortmund msimu ujao. Reus alipata asilimia 35.7 ya kura , akifuatiwa na mchezaji mwenzake wa Borussia Dortmund msimu ujao Mario Goetze ambaye alipata asilimia 12.7, pamoja na mshambuliaji wa Bayern Munich, Frank Ribery, akipata asilimia 12.2.

Moenchengladbach's Marco Reus celebrates after scoring during the German first division Bundesliga soccer match between Borussia Moenchengladbach and FC Schalke 04 in Moenchengladbach, Germany, Sunday, Feb. 20, 2011. (AP Photo/Martin Meissner) ** NO MOBILE USE UNTIL 2 HOURS AFTER THE MATCH, WEBSITE USERS ARE OBLIGED TO COMPLY WITH DFL-RESTRICTIONS, SEE INSTRUCTIONS FOR DETAILS **
Mchezaji bora wa msimu huu Marco Reus wa Borussia MoenchengladbachPicha: AP

Dortmund imetoa kitita cha euro milioni 17.1 kupata saini ya mchezaji huyo wa kiungo wa Moenchengladbach ambaye amekwisha tupa wavuni mabao 10 hadi sasa katika msimu huu.

Na huko katika bara la Afrika , michuano ya kuwania ubingwa wa mataifa ya bara hilo inatarajiwa kutimua vumbi kuanzia Januari 21 siku ya Jumamosi. Kocha wa Sudan, Mohammed Abdallah, anaamini kuwa timu yake inaweza kufikia robo fainali ya michuano hiyo ya kombe la mataifa ya Afrika 2012, kinyume na matarajio ya wengi.

Ikiwa pamoja na timu inayopigiwa upatu kutoroka na kombe hilo Cote D'Ivoire , Angola na Burkina Faso mjini Malabo katika kundi B, wengi wa wadadisi wa masuala ya soka wanaamini kuwa timu hiyo kutoka Afrika mashariki itakuwa na bahati iwapo itaepuka kipigo mara tatu.

Abdallah, kocha wa Sudan, ambaye amefanikiwa kufikisha mwisho ukame wa miaka 32 wa kutoshiriki katika kinyang'anyiro hicho mwaka 2008, anatofautiana na mawazo hayo katika mahojiano aliyoyafanya ndani ya nje ya nchi yake kabla ya mashindano hayo yanayofanyika nchini Gabon na Guinea ya Ikweta.

Angola inalenga kuingia pia katika robo fainali ya mashindano hayo ikiwa ni lengo lao kuu katika michuano ya mwaka huu nchini Gabon na Guinea ya Ikweta.

Baada ya kutolewa mara tatu katika duru za awali , Palancas Negros , ama Paa mweusi , walifikia robo fainali ya mwaka 2008 , na kufungwa kwa taabu na walioibuka mabingwa wa michuano hiyo Misri mjini Kumasi na kisha kutolewa na Ghana mjini Luanda mwaka 2010.

Angola inaanza kampeni yake hiyo kwa kukwaana na Burkina Faso katika uwanja wenye uwezo wa kujaza watazamaji 15,000 wa Nuevo Estadio Malabo , ambao ni uwanja mdogo kabisa kwa mashindano haya ya kombe la Afrika katika historia ya hivi karibuni.

Nae mshambuliaji wa kimataifa wa Cameroon, Samuel Eto'o, ambaye timu yake inakosekana mwaka huu katika kinyang'anyiro cha kombe la mataifa ya Afrika, amesema ana nia ya kubakia katika klabu ya premier league ya Urusi ya Anzhi Makhachkala hadi atakapomaliza muda wake wa kucheza soka.

Sijafikiria kuihama Makhachkala tangu nimefika hapa. Hakuna hata sekunde moja , mchezaji huyo ambaye aliwahi kuwa mchezaji bora kwa mara nne wa bara la Afrika alinukuliwa akisema wiki hii.

Champions League FC Bayern Inter Mailand Samuel Eto'o
Samuel Eto'o wakati akiwa Inter Milan akijaribu kumtoka mchezaji wa Bayern Munich daniel BuytenPicha: picture alliance/dpa

Mshambuliaji Ronaldinho wa Brazil ametishia kujitoa kutoka katika klabu yake ya Flamenco hadi pale atakapopokea kiasi cha dola milioni mbili ambazo ni mshahara wake ambao hajalipwa, amesema wakala wake ambaye ni kaka yake, Roberto de Assis.

Nataka kufikia makubaliano na kisha atashiriki katika kopa Libertadores. Lakini sifikiri iwapo hilo litatokea , de Assis ameliambia gazeti la Extra kabla ya mchuano wa hapo Januari 25 dhidi ya timu kutoka Bolivia ya Real Potosi.

Robo tatu ya mshahara wa Ronaldinho inapatikana kutoka kwa kampuni la matangazo ya biashara la Traffic, ambalo halijalipa mshahara huo kwa muda wa miezi mitano na kufikia kiasi cha dola milioni 2.5.

Meneja wa maendeleo wa kamati ya kimataifa ya Olympiki kwa wachezaji wenye ulemavu, Carolin Rickers, amesema kuwa uwezo mkubwa ulioonyeshwa na Rwanda katika michezo ya Olympiki kwa walemavu ilikuwa ni sababu muhimu ya nchi hiyo kuteuliwa kufanya mradi maalum wa kimataifa kwa ajili ya michezo ya walemavu katika mataifa ya Afrika ya mashariki na kati .

Kiasi ya vijana 70 wenye umri wa miaka 16-25 kutoka Uganda, Kenya, Tanzania, Burundi, jamhuri ya kidemokrasi ya Congo na Rwanda watapiga kambi nchini humo kuazia February 12-18 kupata mafunzo zaidi.

Nilizungumza na rais wa kamati ya taifa ya Olimpiki kwa michezo ya walemavu nchini Rwanda Dominique Bizimana , na nilimuuliza iwapo ni mradi gani unaofanyika kwa vijana hao.

Ufilipino imesema wiki hii kuwa itatuma kikosi kidogo kabisa katika ujumbe wa michezo ya Olimpiki mjini London ambapo itakuwa na wanariadha watano tu kutoka katika taifa hilo ambalo ni la 12 kwa wingi wa idadi ya wakaazi duniani.

Msemaji wa kamati ya olimpiki ya Ufilipino, Joey Romasanta, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa mpiga masumbwi Mark Antony Barriga na kwamba kila nchi inapaswa kutuma mwanamke na mwanamume katika riadha na kuogelea.

Nae Ian Thorpe bingwa mara tano wa olimpiki ameshindwa kufuzu katika mchezo huo wa kuogelea katika mashindano yaliyofanyika mjini Melbourne wiki hii nchini Australia.

Na kwa taarifa hiyo mpendwa msikilizaji sina la ziada ila ni kukuaga kutoka kipindi hiki cha michezo kwa leo. Ahsante kwa kuniazima sikio lako wakati wote huo na hadi mara nyingine kwaherini.

Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae/afpe/rtre

Mhariri: Othaman Miraji