1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Libya: Jibril aongoza matokeo ya awali

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa Libya yanaonyesha kwamba chama cha kiliberali cha NFA cha waziri mkuu wa zamani wa waasi wakati wa vita dhidi ya utawala wa Muammar Gaddafi, Mahmud Jibril, kimepata kura nyingi zaidi.

Kiongozi wa chama cha NFA, Mahmud Jibril

Kiongozi wa chama cha NFA, Mahmud Jibril

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa Libya yanaonyesha kwamba chama cha Mahmud Jibril kimepata kura nyingi zaidi na hivyo kuvipita vyama vya waislamu wenye itikadi kali. Matokeo haya ni tofauti na chaguzi zilizofanyika hivi karibuni nchini Tunisia na Misri ambapo vyama vya Udugu wa Kiislamu viliweza kujipatia wingi wa kura. Matokeo rasmi ya uchaguzi yanatarajiwa kutolewa mnamo wiki ijayo. Lakini kwa sasa sehemu kubwa ya kura imeshahesabiwa na inaonekana kwamba chama cha National Forces of Alliance, kinaongoza katika mji mkuu Tripoli, maeneo ya kusini mwa Libya na vile vile katika mji wa Benghazi uliokuwa ngome kuu ya upinzani dhidi ya utawala wa miaka 42 wa Muammar Gaddafi. Chama hicho kimepata kura 46,000 katika mji wa Tripoli huku chama cha Justice and Construction Party (JCP) cha Udugu wa Kiislamu kikiambulia kura 4,700 tu.

Kura bado zinaendelea kuhesabiwa Libya

Kura bado zinaendelea kuhesabiwa Libya

Nasser Ahdash, ambaye ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Libya ameeleza kwamba raia wa nchi hiyo wanamchukulia Jibril kama alama ya kuwa wazi kwa dunia nzima na kwamba huu ni uwazi ambao wamekuwa wakiutamani baada ya kufungiwa ndani na mtawala wa zamani Gaddafi kwa miaka mingi. "Nimempigia kura Jibril na sasa ninatumaini kwamba Libya itakuwa na mustakabali mwema. Matokeo yanaonyesha kwamba chaguo langu lilikuwa sahihi," alieleza Ayman Abuda, mwanamke mwenye umri wa miaka 35 kutoka Tripoli."

Wabunge kuchaguliwa mwakani

Vyama vya upinzani havina nafasi ya kukata rufaa kupinga matokeo ya uchaguzi hadi matokeo rasmi yatakapotolewa. Hata hivyo, ushindi wa Jibril haumaanishi kwamba chama chake kitakuwa na wabunge wengi zaidi katika baraza la wawakilishi la nchi yake lenye viti 200. Hii ni kwa sababu viti 120 vimewekwa kwa ajili ya wagombea huru ambao haifahamiki hasa wanaegemea upande upi. Baraza hilo litamchagua kwanza waziri mkuu pamoja na baraza la mawaziri na kisha kuandaa uchaguzi wa wabunge utakaofanyika mwaka kesho. Mahmud Jibril huenda akawa kiongozi mpya wa Libya na kulingana na aina ya serikali ambayo nchi yake itamua kuwa nayo, anaweza hata kuwa rais.

Jibril, mwenye umri wa miaka 60, amevitaka vyama vyote vya nchini mwake vikae pamoja ili kuunda serikali ya umoja wa kitaifa yenye lengo la kuijenga upya nchi hiyo. Wachambuzi wanaeleza kwamba Jibril ndiye mtu anayefaa kuufufua uchumi wa Libya ambao kwa sehemu kubwa unategemea mauzo ya mafuta.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/Reuters/afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman