Leo ni Siku ya Uchaguzi mkuu Ujerumani | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 27.09.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Leo ni Siku ya Uchaguzi mkuu Ujerumani

Wapiga kura wamiminika kuchaguwa Bunge la Ujerumani

default

Kansela Angela Merkel akiwahutubia wananchi katika kampeni ya uchaguzi

Wajerumani milioni 62 kote nchini wameanza kupiga kura leo tangu saa mbili za asubuhi, saa tatu huko Afrika Mashariki, katika uchaguzi ambao unaonekana utamrejesha Kansela Angela Merkel madarakani, lakini huenda ukamnyima kupata serekali ya mrengo wa kati na kulia ambayo anasema anaihitaji ili kuufufua uchumi wa nchi yake ulio mkubwa kabisa barani Ulaya. Ni wazi kwamba Bibi Merkel, kama mtetezi wa chama chake cha CDU/CSU, atamtangulia mshindani wake kwa wadhifa wa ukansela kwa tiketi ya Chama cha SPD, waziri wa mambo ya kigeni wa sasa, Frank-Walter Steinmeier, lakini kuna walakini nyingi kuhusu mfumo wa serekali ijayo itakayotawala hapa Ujerumani mnamo miaka minne ijayo.

Miaka minne baada ya kuchukuwa madaraka, akiongoza serekali ya mseto ya vyama vikubwa, CDU/SCSU na SPD, Bibi Merkel anakubalika sana mbele ya wananchi. Lakini baada ya kuendesha kampeni ambayo watu wengi wameilaumu kuwa ni chapwa, inayokosa msisimko na haijazungumzia masuala yanayowagusa wananchi, Chama cha Christian Democratic, CDU, cha Bi Merkel kimeshuhudia umbele wao, kwa mujibu wa taasisi za uchunguzi wa maoni ya watu, unayayuka mnamo wiki za hivi mwishoni. Sasa sio hakika kama ataweza kuunda serekali ya mseto anayoitamani baina ya chama chake na kile cha kiliberali cha FDP. Pindi mambo yatakuwa hivyo, basi itambidi aunde serekali kama hii ya sasa alioiongoza tangu mwaka 2005 baina ya chama chake na Chama cha Social Democratic, SPD.

Moja kwa tano ya wapiga kura walikuwa hawajaamuwa hadi alfajiri ya leo chama gani watakichagua, hivyo kuengeza uwezekano wa kutokea maajabu pale vituo vya uchaguzi vitakapofungwa leo saa kumi na mbili za jioni.

Jana, katika mkutano wa hadhara wa kampeni yake, Bibi Merkel alisema:

"Kesho ni kuonesha kwamba Chama chetu cha CDU kina nguvu; nasema ni vyama vikuu pekee vya CDU na CSU vilivo na nguvu kuweza kuunda serekali yenye mwelekeo mpya, lakini mwelekeo ambapo sisi ni wenye nguvu. Ni sisi tu tunaoweza kuwakilisha siasa za katikati katika jamii yetu."

Hivyo, hadi jana jioni, vyama viku vya kisiasa vilikuwa vinajaribu kuwavutia watu ambao bado hawajaamuwa kura zao watakipa chama gani. Katika mji wa Dresden, mtetezi wa ukansela kwa Chama cha SPD, Frank-Walter Steinmeier alisema:

"Nyinyi mnajuwa na mnakumbuka mwishowe mambo yanakuwa mengine. Mara hii vile vile itakuwa vivyo hivyo

Bundestagswahlen 2009 Stimmabgabe Frank-Walter Steinmeier

Mtetezi wa ukansela kwa tiketi ya Chama cha Social Democratic, SPD, Fran-Walter Steinmeier, akitumbukiza kura yake katika sanduku la uchaguzi wa Ujerumani hii leo

Lakini yaonesha Frank-Walter Steinmeier ameshapoteza matumaini kwamba chama cha kiliberali cha FDP kitataka kuungana na chama chake cha SPD...

" Bibi Merkel ameamuwa. Yeye anataka kuwana serekali ya CDU na FDP. Ikiwa ni ni hivyo kitakachoonekana ni kile kilichoshuhudiwa katika miaka ya tisini, yaani kupunguziwa kodi watu walio wachache, kupunguzwa huduma za kijamii kwa watu wengi na hapa nasema : kusambaratika nchi yetu. Jambo hilo lazima tulizuwie."

Baada ya kuwemo serekalini kwa miaka 11, uchunguzi wa maoni ya watu, hata hivyo, unatabiri kwamba Chama cha SPD kitakusanya kura chache kabisa kuwahi kujipatia tangu mwaka 1945.

Uchaguzi huu unafanyika katika wakati muhimu kwa Ujerumani, nchi hii ikiwa inajikokota kutoka hali ya uchumi wake kwenda chini sana, jambo ambalo halijawahi kushuhudwa tangu vita vikuu vya pili vya dunia. Bibi Merkel katika kuwavutia wapiga kura, alidokeza kupunguza kodi za mapato:

"Yule ambayo anapata mshahara zaidi, lazima ahisi hali hiyo katika mfuko wake, lazima kile kinachobakia baada ya kulipa kodi kiwe kikubwa. Yule anayefanya kazi, lazima awe na fedha zaidi kuliko yule asiyefanya kazi. Kufanya kazi kwa bidii lazima kuwe na faida..."

Lakini Chama cha kiliberali cha FDP kinachoongozwa na Guido Westerwelle kinatajwa kwamba kitafanya vizuri, hivyo, baada ya miaka 11 huenda kikasita tena kuwa chama cha upinzani. Ni vyama vitano tu, CDU/CSU, SPD,FDP, Chama cha Kijani na kile cha mrengo wa shoto, Die Linke, vinavotarajiwa kuvuka kiunzi cha asilimia tano ya kura kuweza kuwakilishwa bungeni.

Guido Westerwelle / FDP

Guido Westerwelle, mkuu wa Chama cha kiliberali cha FDP, akihutubia mkutano wa mwisho wa kampeni za uchaguzi wa Ujerumani kwa ajili ya chama chake

Lakini kutokana na mfumo wa uchaguzi ulivyo hapa Ujerumani, Chama cha CDU huenda kikafaidika na hadi viti 20 katika bunge lilopangiwa kuwa na wajumbe 598 kutoka na vile vinavoitwa viti vya ziyada.

Bibi Angela Merkel katika kampeni zake za uchaguzi ameahidi kuufufua na kuuimarisha uchumi, na jambo hilo amesema ataweza kulitekeleza kwa uzuri akishirikiana na Chama cha FDP. Chama cha SPD kimeandaa mpango kabambe wa kuunda nafasi za kazi milioni nne, ambazo zitatokana na kile kinachoitwa teknolojia ya kuboresha mazingira. Vyama vya CDU na FDP vinapanga kurefusha muda kabla ya kuvifunga vinu vya kinyuklya, ambavyo vyama vya SPD na kile cha Kijani vinataka vifungwe ifikapo mwaka 2020.

Chama cha mrengo wa kulia, Die Linke, mabaki ya chama cha zamani cha kikoministi cha iliokuwa Ujerumani mashariki, bado kinaungwa mkono na watu wengi katika mikoa ya Mashariki ya Ujerumani na kimewavutia wanachama wa zamani wa SPD ambao hawafurahishwi na siasa za SPD zinazoelemea mrengo wa katikati. Kiongozi wa chama hicho, Oskar Lafontaine amesema:

Oskar Lafontaine Wahlparteitag Die Linke

Oskar Lafontaine, mkuu wa Chama cha mrengo wa shoto cha Die Linke, akihutubia katika kampeni ya uchaguzi ya chama chake"Watu wengi wanasema Chama cha CDU na FDP visiwe na wingi bungeni, na jambo hilo ni muhimu kwa ajili ya Ujerumani. Isiruhusiwe kwamba vyama vitakavounda serekali viwe vile ambavyo vinabeba dhamana ya mzozo wa sasa."

Vyama vya kisiasa hapa Ujerumani havimudu kuwadharau wazee, kwani wapiga kura walio zaidi ya umri wa miaka 60, ni thuluthi moja ya wapiga kura. Hata hivyo, wapiga kura vijana milioni 3.5 watatapiga kura leo kwa mara yao ya kwanza.

Ulinzi umezidishwa kote hapa Ujerumani katika siku ya leo ya uchaguzi, na hasa kutokana na vitisho vilivotolewa karibuni katika kanda za video za Waislamu wenye siasa kali, kutoka mtandao wa kigaidi wa al-Qaida na Wataliban, zikitaka Ujerumani iondoshe majeshi yake kutoka Afghanistan.

Katika uchaguzi uliopita hapo mwaka 2005, chama cha CDU/CSU kilipata asilimia 35 ya kura, wakati FDP ilinyakuwa asilimia 10. Chama cha SPD kilizoa asilimia 35, chama cha mrengo wa Shoto cha Die Linke asilimia tisa na kile cha Kijani asilimia nane.

Mara hii ukweli utajulikana leo baada ya saa kumi na mbili za jioni.

 • Tarehe 27.09.2009
 • Mwandishi Miraji Othman/Reuters/dpa/AFP
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/JpwV
 • Tarehe 27.09.2009
 • Mwandishi Miraji Othman/Reuters/dpa/AFP
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/JpwV

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com