1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lebanon yapata serikali mpya

16 Februari 2014

Waziri mkuu wa Lebanon Tammam Salam jana Jumamosi(15.02.2014) ametangaza serikali ya maridhiano, baada ya miezi 10 ya mvutano wa kisiasa ambao vita katika nchi jirani ya Syria ulizidisha wasi wasi wa kimadhehebu.

https://p.dw.com/p/1B9u4
Libanon Regierung Beirut 15.2.2014
Serikali ya LebanonPicha: picture-alliance/dpa

Serikali hiyo itakayokuwa na mawaziri 24, na inayojumuisha mwanamke mmoja, inayaleta pamoja makundi yenye ushawishi, kundi la Washia la Hezboullah na washirika wake pamoja na kundi linaloongozwa na Wasunni la waziri mkuu wa zamani Saad Hariri, makundi ambayo yanaunga mkono pande tofauti katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

"Baada ya juhudi za miezi 10 , za uvumilivu, serikali itakayokuwa inalinda maslahi ya taifa imezaliwa," amesema Salam , ambaye alipewa jukumu la kuunda serikali mwezi Aprili mwaka jana.

Tammam Salam Libanon Regierung Beirut 15.2.2014
Waziri mkuu Tammam SalamPicha: picture-alliance/AA

"Ni serikali inayoleta umoja na mfumo bora kabisa wa kuruhusu Lebanon kupambana na changamoto," alisema Salam wakati akitangaza orodha ya mawaziri katika serikali hiyo itakayochukua nafasi ya serikali ya mtangulizi wake Najib Mikati.

Ghasia zimevuka mipaka

Vita vya Syria vya karibu miaka mitatu vimeigawa kwa kiasi kikubwa Lebanon , na ghasia zimevuka mipaka na kuingia ndani ya nchi hiyo ndogo katika bahari ya Mediterranea, ambayo imekumbwa na mashambulizi kadha ya mabomu yakutegwa katika magari pamoja na mashambulizi ya kujitoa muhanga.

Lebanon pia inapitia katika kipindi kigumu kwa kuwahifadhi zaidi ya wakimbizi milioni moja kutoka Syria , ambao wanatoa changamoto kwa rasilmali ambazo tayari ni ndogo nchini humo.

Salam ameahidi "kuimarisha usalama , kupambana na vitendo vya aina yoyote vya kigaidi" na kupambana na "mzigo" unaoikabili Lebanon wakati wakimbizi zaidi wakimiminika kutoka Syria.

Drei Tote bei Bombenanschlag in Hermel, Libanon
Shambulio la bomu mjini BeirutPicha: Getty Images/AFP

Tangu mwezi Aprili mwaka jana, juhudi za kuunda serikali zimekwaa visiki kutokana na mizozo kati ya hezboullah , ambayo wapiganaji wake wamekuwa wakiusaidia utawala wa rais Bashar al-Assad kuzima uasi, na kundi la Hariri ambalo linaunga mkono vuguvugu la uasi linaloongozwa na Wasunni.

Uingereza, Ufaransa, Marekani na Umoja wa Ulaya zote zimekaribisha serikali mpya, zikiahidi kufanya kazi pamoja na waziri mkuu Salam pamoja na baraza lake la mawaziri kuisaidia Lebanon kuweza kupata usalama na uthabiti.

Mahasimu waja pamoja

Serikali hiyo mpya inawaleta pamoja kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka mitatu kundi la Hezboullah na la Hariri , na maridhiano yaliyofikiwa yanahakikisha kuwa hakuna upande wenye kura ya turufu dhidi ya upande mwingine.

Wizara 24 zimegawanywa katika makundi matatu, ambapo Hezboullah na kundi la Hariri kila moja linapata wizara nane, na wajumbe wanaoonekana kuwa wasio na upande watapewa nyadhifa zilizobaki.

Kulinda uwiano huo tete kati ya madhehebu 18 ya nchi hiyo, serikali pia imegawanywa sawia kati ya Wakristo na wawakilishi wa makundi ya Kiislamu.

Tawi la kisiasa la Hezboullah litakuwa na mawaziri wawili, waziri wa viwanda na waziri wa nchi anayehusika na masuala ya bunge, na washirika wake wakichukua nyadhifa ambazo ni pamoja na wizara ya mambo ya kigeni na wizara ya nishati.

Mwanamke mmoja tu , Alice Shabtini ambaye anafikiriwa kuwa hana upande , amepewa wadhifa. Ataongoza wizara yenye jukumu la kuwahudumia watu waliokimbia makaazi yao katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1975 hadi 1990.

Syrische Kinder im Flüchtlingslager im Winter
Wakimbizi wa Syria nchini LebanonPicha: AFP/Getty Images

Hariri alisafisha njia kupatikana muafaka wakati alipotangaza kubadilisha msimamo wake mwezi uliopita kwamba atakuwa tayari kuruhusu lile linalojulikana kama kundi lake la Machi 14 kujiunga na serikali pamoja na mahasimu wao wa kundi la Hezboullah.

Wanachama watano wa Hezboullah hivi sasa wanakabiliwa na kesi bila ya kufika mahakamani katika mahakama maalum mjini The Hague kwa madai ya kuhusika katika mauaji ya mwaka 2005 ya baba yake Hariri , ambaye ni waziri mkuu wa zamani Rafik Hariri.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Amina Abubakar