1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kusini mwa Sudan - Mzozo uliosahaulika

Sekione Kitojo17 Agosti 2009

Watu milioni mbili wamepoteza maisha yao na wengine zaidi ya nusu milioni wamekuwa wakimbizi. Hali bado inaonekana kuwa ya wasi wasi hadi sasa.

https://p.dw.com/p/JCi4
Wanajeshi wa jeshi la ukombozi kusini mwa Sudan (SLA) wakifanya doria katika mji wa Muhujariya.Picha: dpa

Watu milioni mbili wameuwawa, milioni nne wamepoteza makaazi yao , zaidi ya nusu milioni wamekuwa wakimbizi nje ya nchi yao, miaka 22 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kusini mwa Sudan , kwa kiasi kikubwa vilikuwa vita vibaya kabisa hata kuliko vita vya hivi sasa katika jimbo la Darfur. Kwa muda wa miaka mitano kumekuwa na makubaliano ya kusitisha mapigano. Imebakia miaka sita kabla ya kufikia mwaka 2011 ambapo watu wa kusini mwa Sudan watapiga kura ya maoni kuamua iwapo wawe taifa huru ama la. lakini inaonekana kuwa kila muda huo unapokaribia, kuna wasi wasi mkubwa wa kuzuka tena vita.

Katika majira ya mchana watu wawili wanaonekana katika mji wa Wao ambao wana jukumu la kulinda amani. Kiongozi ni Renato Soerro kutoka Brazil na meja Abdul-Razak Rashid kutoka Tanzania. Wamevalia sare zao za kijeshi za rangi ya kijivu jivu na kijani, na katika mabega yao ya kushoto wana alama ya umoja wa mataifa. Ni wawili kati ya wanajeshi 10,000 wa jeshi la umoja wa mataifa nchini Sudan. Wamo katika gari lao jeupe wakipita katika mji wa Wao mji wa pili kwa ukubwa katika eneo hilo la kusini mwa Sudan.

Mbele ya lango la ofisi za umoja wa mataifa kuna magunia ya mchanga na nyuma ya magunia hayo kuna wanajeshi wenye silaha. Wanajeshi wa umoja wa mataifa kutoka Kenya wanaanga kwa darubini kuelekea eneo la mjini. Kikosi kinachofanya doria asubuhi hii hakijapata tukio lolote baya. Wao ni eneo tulivu. Ni tofauti na maeneo mengine, anasema Renato Soerro.

Hasa iwapo utakwenda karibu na mpaka, karibu na Abieyi ama kusini mwa Darfur, utaona hali tofauti kabisa kuliko hapa Wao. Kwa sababu ya mipaka na suala la mafuta, pamoja na mapigano ya kikabila, huenda hizi ni sababu ambazo tunaweza kusema Wao ni mji tulivu lakini sehemu nyingine haziko hivi.

Mlinzi huyo wa amani wa umoja wa mataifa anatoa maelezo ya kidiplomasia zaidi. Idadi ni wazi. Kuna watu tayari 100 waliouwawa katika mapambano kati ya makundi tofauti. Athari za vita hivi , ni serikali ya kaskazini mwa Sudan ikiwa na makabila mbali mbali walipopambana na waasi upande wa kusini. Na hata katika mji wa Wao si mara zote kumekuwa na hali ya utulivu kutokana na mkataba huo wa amani. Walinzi hawa wa amani wa umoja wa mataifa wanatambua hilo wakati wakipita katika mji huo. Makao makuu ya jeshi la pamoja kati ya jeshi la serikali na lile lililokuwa la waasi wa SPLA pia yapo katika mji huo. Mkataba wa amani bado unaheshimiwa tangu ulipotiwa saini mwaka 2005. Lengo kuu ni kuwa na jeshi la pamoja.

Tunachokiona hapa ni mazoezi ya viungo, wanafanya pamoja. Lakini ni katika mazoezi ya kawaida, inakuwa si rahisi kuwafanyisha mazoezi ya kijeshi ama mbinu za kijeshi pamoja , lakini ni mazoezi ya kawaida. Na baada ya hapo siku nzima wanabaki wakiwa wamepumzika, na wametenganishwa kati ya wanajeshi wa serikali na wale wa SPLA.

Vipi Wasudan ya kusini wataamua katika kura ya maoni hapo mwaka 2011, wakati muda utakapofika , ni suala la kusubiri na kuona.

Mwandishi Daniel Pelz/ZR/Sekione Kitojo

Mhariri Othman Miraji.