1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura zahesabiwa Jamhuri ya Congo.

Halima Nyanza13 Julai 2009

Zoezi la kuhesabu kura linaendelea leo katika Jamhuri ya Congo baada ya kufanyika uchaguzi wa Rais jana, ambao matokeo yake yanatarajiwa kumrejesha madarakani Rais Denis Sassou Ngueso, huku wapinzani wakipinga.

https://p.dw.com/p/ImGz
Rais anayetetea nafasi yake nchini Jamhuri ya Congo, Denis Sassou Nguesso (kati) akiteta na mchungaji Jesse Jackson wa Marekani.Picha: AP

Ripoti iliyotolewa na nusu ya wagombea 12 wanaompinga Rais Denis Sassou Nguesso, ambaye ametawala taifa hilo la Afrika ya kati lenye utajiri wa mafuta lakini lililo na umasikini katika vipindi tofauti tangu mwaka 1979, imesema kuwa zaidi ya asilimia 90 ya watu wote wenye uwezo wa kupiga kura hawakujitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo wa jana.


Ripoti hiyo imesema kwa hali hiyo raia wa Congo wameeleza wazi kwa kutopiga kura kwa asilimia zaidi ya 90.


Imeongeza kusema kuwa Wacongo ambao wanapenda haki na amani wameelezea kupinga kwao utawala wa kiimla, wenye kutumia vibaya madaraka na utawala ulio na rushwa kwa asilimia kubwa ya watu kutopiga kura.


Ripoti hiyo imelaumu pia vitendo vya udanganyifu na kununuliwa wapiga kura na kwamba wanajeshi walio karibu na Rais huyo wamepiga kura mara kadhaa katika vituo tofauti vya kupigia kura.


Hata hivyo, serikali ya Jamhuri ya Congo ilikanusha kwa haraka madai hayo.


Waziri wa Habari wa nchi hiyo na msemaji wa serikali, Alain Akouala Atipault, amesema tamko hilo la upinzani juu ya udanganyifu mkubwa sio sahihi.


Ameeleza kuwa hawawezi kuongelea udanganyifu wakati nchini humo kuna waangalizi wa kimataifa wapatao 170.


Rais Denis Sassou Nguesso, mwenye umri wa miaka 66, anatafuta tena awamu mpya ya saba madarakani, kwa kuungwa mkono na kundi kubwa la vyama vinavyomuunga mkono bungeni dhidi ya wagombea wengine 12.


Ameiongoza Congo kwa takriban miaka 25, ambapo alishika madaraka kuanzia mwaka 1979 hadi 1992 na kurudi tena katika nafasi hiyo ya urais mwaka 1997, baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.


Sassou Nguesso alichaguliwa tena mwaka 2002 katika uchaguzi ambao waangalizi wa kimataifa walisema ulikuwa na kiwango kidogo cha demokrasia.


Waangalizi wa Umoja wa Afrika nao pia wametambua kuwepo kwa rushwa na ukiukaji wa taratibu za upigaji kura katika uchaguzi wa bunge na wa mitaa katika mwaka 2007 na 2008.


Tume ya Uchaguzi nchini humo imesema matokeo ya uchaguzi wa majimbo yanatarajiwa kutolewa katika siku tatu ama nne zijazo.


Aidha kama hakutakuwa na mgombea wa Urais atakayeshindi kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa, duru ya pili ya uchaguzi itaendeshwa.


Takriban Wacongo milioni 2.2 wana uwezo wa kupiga kura kati ya watu milioni 3.6 nchini humo.


Licha ya mafuta na usafirishaji mkubwa nje wa mbao, asilimia 70 ya wakazi wa nchi hiyo wanaishi katika umasikini mkubwa.


Mwandishi: Halima Nyanza(AFP)

Mhariri: Miraji Othman