1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura za Wahispania na majaliwa ya Obama 2012

Admin.WagnerD3 Mei 2012

Ni dhahiri sasa kuwa Rais wa Marekani Barack Obama atapambana na mwana Republican Mitt Romney katika kinyanganyiro cha uchaguzi wa rais nchini humo Novemba mwaka huu.

https://p.dw.com/p/14ow9
Rais Barack Obama
Rais Barack ObamaPicha: picture-alliance/dpa

Hii ni baada ya Newt Gingrich kujiondoa katika kinyanganyiro cha kutafuta mshika bendera ya chama cha Republican siku ya Jumatano. Obama anaweka karata yake kwa wapiga kura wenye asili ya Hispania ambao ndiyo kundi linalokuwa kwa kasi zaidi nchini Marekani, kuweza kumshinda Mitt Romney.

Asimilia kubwa ya kundi hili wanamuunga mkono rais Obama ikilinganishwa na wale wanaomuunga mkono Romney, na kura yao itakuwa muhimu katika kuamua matokeo ya jumla hapo Novemba 6.

Mitt Romney
Mitt RomneyPicha: AP

Umuhimu wa Wahispania unatokana na mfumo wa jimbo kwa jimbo unaotumika kumchagua rais nchini Marekani na wanatizamiwa kumpa ushindi Obama katika majimbo muhimu kama vile Colorado, Nevada na Florida. Zaidi ya hapo, kura ya wahispania inaweza kulirudisha upande wa Obama, jimbo la Arizona ambalo limekuwa chini ya Republicans kwa miaka mingi.

Michelle Obama apima kina cha maji
Mke wa Obama, Michelle alikuwa Arizona siku ya Jumatatu kupima umaarufu wa mume wake katika harambee. Michelle alisimama pia katika majimbo matatu yaliyo na wahispania wengi zaidi kusini magharibi mwa Marekani ambayo ni Colorado, Nevada na New Mexico.

Makamu wa Rais Joe Biden naye alikuwa Arizona wiki mbili zilizopita kujaribu kuwashawishi wapiga kura ambao mara ya mwisho kumchagua mgombea wa Demcrats ilikuwa mwaka 1996 wakati Bill Clinton alipochaguliwa kwa muhula wa pili.

Kihistoria, wahispania ni wafuasi wa chama cha Democrat kutokana na namna chama hiki kinavyoshughulikia suala la uhamiaji ambalo wanalipa kipaumbele cha juu kabisaa. Wanaonekana kuendelea kumuunga mkono Obama licha ya ukweli kuwa chini ya utawala wake, idadi kubwa zaidi ya wahamiaji haramu imerudishwa makwao.

Michelle Obama
Michelle ObamaPicha: AP

Taarifa kutoka Wizara ya mambo ya ndani nchini humo zinaonyesha kuwa tangu mwaka 2009, wahamiaji 400,000 wamerudishwa kila mwaka. Hii ni zaidi ya wale waliorudishwa chini ya utawala wa George Bush.

Kura ya hivi karibuni iliyoendeshwa na kituo cha Utafiti wa watu na vyombo vya habari cha Pew, inaonyesha kuwa Obama anamshinda Romney kwa asilimia 67 kwa 27 miongoni mwa wahispania waliojiandikisha kupiga kura.

Kisa cha Wahispania kutompenda Romney
Romney amejitenga na Wahispania wengi kwa kuunga mkono sheria kali ya uhamiaji iliyopitishwa na jimbo la Arizona na kusema kuwa inafaa kutumika Marekani kote. Sheria hii iliyopitishwa mwaka 2010 inapingwa vikali na Wahispania na makundi ya haki za wahamiaji.

Romney pia anapinga muswada wa sheria ujulikanao kama Dream Act Legislation ulioadaliwa na chama cha Democrat ambao utawasafishia njia ya kupata uraia, watoto wa wahamiaji haramu kwa masharti ya kuhudumia jeshini au kwenda shuleni.

Obama alishinda katika majimbo ya Colorado, Nevada na Florida mwaka 2008 na kubakiza majimbo hayo kutakuwa muhimu katika uchaguzi wa mwaka huu. Ikiwa ni miezi sita tu iliyosalia kufanya uchaguzi, kura za maoni kitaifa zinaonyesha wawili hawa wanakaribiana sana, na jambo kubwa katika agenda ni uchumi. Hii inazidi kuifanya kura ya wahispania iwe na umuhimu zaidi kwa Obama.

Makamu wa Obama Joe Biden
Makamu wa Obama Joe BidenPicha: dapd

Kama uchaguzi ungefanyika leo
Utafiti unaonyesha kama uchaguzi ungefanyika leo, Obama angeshinda kwa urahisi katika majimbo 14 ya Democrats hususani katika pwani za mashariki na magharibi pamoja na Wilaya ya Columbia kwa jumla ya kura za uchaguzi186 na Romney angeshinda katika majimbo 20 ya republicans yenye jumla ya kura za uchaguzi 156.

Kura za majimbo (electrol votes) zina nguvu zaidi kuliko kura za wananchi (popular votes). Mwaka 2000 mgombea wa Democrats Al-Gore alishinda kura za wananchi lakini alipoteza kwa George Bush aliyeshinda kura za majimbo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\APE
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman.