Kura ya maoni yaendelea kusini mwa Sudan
11 Januari 2011Kura ya maoni nchini Sudan kuhusu eneo la kusini lijitenge ama la imeendelea kuwa na milolongo mirefu ya wapiga kura katika siku yake ya pili lakini imechafuliwa pia na mivutano ambayo imesababisha maafa katika jimbo la Abyei. Machafuko hayo yamesababisha kiasi watu 23 kupoteza maisha tangu siku ya Ijumaa. Vikosi vya kulinda amani vya umoja wa mataifa vimepelekwa katika eneo hilo kufanya uchunguzi katika jimbo la mpakani, ambako kura ya maoni kuhusu hatma ya eneo hilo imeahirishwa. Viongozi wa kabila la Dinka, ambao wanapendelea kuwa upande wa kusini, wameishutumu serikali ya upande wa kaskazini mjini Khartoum kwa kuwapa silaha Waarabu wafugaji katika jimbo la Abyei. Msemaji wa jeshi la Sudan ya kaskazini amekanusha kuhusika kwa aina yoyote na machafuko hayo. Kwingineko nchini Sudan , jana Jumatatu, maelfu ya wapiga kura walijipanga kwa amani kupiga kura. Kura hiyo ya maoni itafanyika kwa muda wa wiki nzima. Ni kilele cha makubaliano ya amani ya mwaka 2005 ambayo yamemaliza miongo miwili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta.