Kura ya maoni Sudan ya kusini
9 Januari 2011Baada ya miaka 50 ya mzozo ulioleta maafa makubwa, watu wa Sudan ya kusini hatimaye wanapiga kura hii leo kuamua iwapo waendelee kuwa sehemu ya Sudan moja ama kujitenga na kuwa taifa la 193 duniani. Mpendwa msikilizaji natumai kuwa nawe kwa muda wa dakika hizi tano kuangalia maandalizi ya siku hii ya kihistoria katika bara la Afrika.
Upigaji kura unaanza rasmi saa kumi na mbili asubuhi katika siku saba za kwanza za upigaji kura katika kura ya maoni ambayo ni ya kihistoria ambayo ni kilele cha makubaliano ya amani ya mwaka 2005 kati ya upande wa kaskazini na kusini na kumaliza vita vilivyochukua muda mrefu zaidi katika bara la Afrika.
Hali ya shauku imeukumba mji mkuu wa eneo la kusini wa Juba katika mkesha wa upigaji kura wakati watu wa eneo hilo wakifurahia kujitokeza kwa saa za mwisho za mzozo uliochukua muda mrefu na wakati mwingine ulioonekana kuwa mgumu.
Mcheza sinema nyota kutoka Marekani George Clooney amejiunga na viongozi waliopo madarakani na wale wa zamani wa mataifa ikiwa ni pamoja na seneta mwandamizi wa bunge la Marekani John Kerry , rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter na katibu mkuu wa zamani wa umoja wa mataifa Kofi Annan katika mji huo kwa ajili ya siku hii muhimu kwa watu wa Sudan ya kusini.
Lakini sherehe hizo zilichafuliwa kidogo na mapigano kati ya makundi ya kikabila yenye silaha pamoja na wanamgambo waliojitenga katika maeneo mawili yanayozalisha mafuta katika mpaka wa kaskazini na kusini maeneo ambayo yalikuwa yakigombaniwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1983 hadi 2005.
Rais wa kusini mwa Sudan Salva Kiir amewaambia watu wa eneo hilo katika mkesha wa kupiga kura kuwa hakuna kitu mbadala ila kuishi kwa amani na upande wa kaskazini wa Sudan.
Amesema kuwa , tumebakiwa tu na saa chache kufanya uamuzi muhimu katika maisha yetu. Hii leo hakuna nafasi ya kurejea katika vita, amesema katika hotuba yake kabla ya kuanza kwa kura hiyo ya maoni.
Mjumbe wa Marekani alikuwa akiongoza juhudi za kimataifa za kidiplomasia hadi katika dakika za mwisho kuhakikisha kuwa kura hiyo ya maoni inafanyika kama ilivyopangwa chini ya makubaliano hayo. Mjumbe wa Marekani nchini Sudan Scott Gration amefanya ziara 24 katika eneo hilo katika juhudi hizo za kidiplomasia.
Mzozo huu baina ya eneo la kaskazini ambalo wakaazi wake wengi ni Waarabu , Waislamu na upande wa kusini ambao wengi ni Waafrika weusi , na ambao ni Wakristo, umeigawa Sudan tangu nchi hiyo kupata uhuru kutoka Uingereza mwaka 1956, ukichochewa na udini, ukabila, siasa na rasilmali, hususan mafuta.
Wasudan ya kusini wanapiga kura hii ya maoni wakiwa katika sehemu mbali mbali, ambazo ama wamekimbilia wakati wa vita, ama wamehamia wakati mwingine. Miongoni mwa sehemu ambapo kura ya maoni inafanyika pia ni nchini Kenya, ambako kuna Wasudan ya kusini wapatao 200,000. Nilizungumza na mwandishi wetu habari kutoka Nairobi Kenya Alfred Kiti kuhusu hali ilivyo na wapiga kura wanatarajiwa kuanza saa ngapi kupiga kura.
Mwandishi: Sekione Kitojo/AFPE
Mpitiaji: Maryam Abdalla