1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya maoni kuhusu kujitenga kwa Sudan kusini huenda icheleweshwe

20 Oktoba 2010

Waziri wa ulinzi wa Sudan, Abdel Rahim Mohamed, amesema kura ya maoni kuhusu kujitenga kwa Sudan Kusini huenda ikahitaji kucheleweshwa hadi matatizo ya mipaka na usalama yatakapotatuliwa

https://p.dw.com/p/Picb
Rais wa Sudan, Omar Hassan al-BashirPicha: picture-alliance/ dpa

Kauli ya waziri wa ulinzi wa Sudan, Abdel Rahim Mohamed ni mapendekezo mazito kuwahi kutolewa na afisa wa ngazi ya juu katika chama tawala nchini Sudan cha National Congress, ya kutaka kura ya maoni ya Januari 9 mwakani icheleweshwe.

Waziri Hussein aliwaambia waandishi habari hapo jana mjini Cairo Misri kwamba kwa kuzingatia hali halisi ilivyo nchini Sudan, kuna haja ya kuiharisha kura hiyo ya maoni. Waziri huyo aidha amesema masuala ya mipaka na eneo la Abyei lazima yatatuliwe kwa misingi ya katiba ya taifa la Susan. Kilicho muhimu ni usalama na uthabiti wa Wasudan, amesema waziri huyo.

Waziri Abdel Rahim Mohamed amesema amejadiliana na rais wa Misri, Hosni Mubarak mjini Cairo kuhusu matatizo yanayotishia kukwamisha kura hiyo ya maoni ya Januari 9 mwakani. Maandalizi ya kura ya maoni yamechelewesha. Raia wa Sudan kusini wakiongozwa na chama kidogo serikalini cha Sudan People´s Liberation Movement, wana msimamo tofauti na raia wa kaskazini kuhusu masuala muhimu kama vile hatima ya mpaka kati yao.

Msemaji wa jeshi la Sudan kusini, Kuol Diem Kuol amesema waziri Hussein hafahamu ukweli halisi wa kusini, akisitiza kuwa wananchi wa eneo hilo wanataka kura hiyo ya maoni ifanyike kama ilivyopangwa, na wala sio kama wanavyotaka madikteta wa mji mkuu, Khartoum.

Wakati huo huo, jeshi la Sudan Kusini limeushutumu Umoja wa Mataifa kwa kushindwa kuripoti kuhusu kuongezeka kwa idadi ya wanajeshi wa kaskazini katika eneo la mpaka baina ya pande hizo mbili, hivyo kuashiria kuwa vita huenda vikazuka. Kiongozi wa ngazi ya juu wa jeshi la Sudan Kusini, Mat Paul amesema jeshi la Sudan kaskazini linawazuia wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kusimamia mkataba wa usitishwaji mapigano na maafisa wa umoja huo hawasemi ukweli kuhusu hali hiyo.

Paul ambaye ni muwakilishi wa jeshi la Sudan kusini, SPLA, katika tume ya pamoja kati ya Susan kusini na kaskazini inayosimamia mkataba wa amani, amesema ongezeko la wanajeeshi wa kaskazini lilianza tangu mwezi Juni mwaka huu katika eneo la Kordofan Kusini na maeneo mengine na wamekuwa wakilizunguzia suala hilo na Umoja wa Mataifa. Jeshi la Sudan kaskazini limekanusha kupeleka vikosi vyake katika eneo la kusini, lakini halijatoa tamko lolote kuhusu madai kwamba linawazuia walinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Rais wa Sudan, Omar Hassan al Bashir, ameapa jana kwamba Sudan haitotumbukia tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, akisema serikali inafanya juhudi kulinda amani na kwamba kura ya maoni haitakuwa mwisho wa dunia.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/RTRE

Mhariri: Aboubakar Liongo