Kura ya kombe la dunia 2010 Durban | Michezo | DW | 26.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Kura ya kombe la dunia 2010 Durban

Uingereza imeangukia kundi moja tena na Croatia.Ujerumani kundi moja na Russia na Finland

default

Rais wa FIFA Sepp Blatter na Thabo Mbeki

Kura kwa kombe la dunia 2010 nchini Afrika kusini imepigwa jana mjini Durban,nani kaangukia kundi gumu na nani kundi hafifu –tutasikia uchambuzi tangu kanda ya Ulaya hata ya Afrika.

Uwezo wa Afrika kusini hasa; na Afrika kwa jumla, kuandaa kombe la dunia la dimba-FIFA World cup-ambao ulitiliwa shaka, ulithibitika jana pale kura ya kuzipambanisha timu kiasi 200 za takriban mabara yote isipokua Amerika kusini, ilipopigwa huko Durban,Afrika kusini.

Rais wa FIFA Sepp Blatter,aliondosha shaka shaka zote aliponadi wazi jana kwamba Kombe la dunia 2010 litaandaliwa Afrika.yeye aliwanyamazisha wale wote waliweka shaka shaka.Hata kamati ya maandalio ya kombe la dunia LOC haitalipuuza onyo la rais wa FIFA Sepp Blatter alipohadharisha kwamba ikiwa kiwanja chochote hakitamalizika kwa wakati,uwanja mwengine utachukua jukumu hilo.

Katika makundi yote 9 ya kanda ya Ulaya kwa kombe la dunia 2010,msangao ulikuja katika kundi la 6 . Uingereza iliopigwa kumbo na Croatia nje ya finali za kombe la Ulaya hapo juzi tu kwa mabao 3-2,imeangukia kundi moja na na Croatia tena.Na alieumwa na nyoka, akiona un’gongo tena hustuka.Croatia si un’gongo kwa Uingereza,bali ni nyoka alieiuma.Timu nyengine katika kundi hili ni Ukraine,Belarus,Kazakhstan na Andora.

Kiongozi wa FA chama cha mpira cha uingereza kinachomsaka bado kocha mpya alieleza hivi juu ya kura ya jana huko Durban:

“ni kundi la kuvutia na ni wazi tuna kazi kubwa ya kufanya katika kundi hili.Kwahivyo, tuna kibarua kigumu mbele yetu.”

“Ujerumani,imeangukia kundi la 4: pamoja na Russia,Finland,Wales,Azerbaijan na Liechtenstein.

Ujumbe wa Ujerumani mjini Durban jana, ulijumuisha Franz Beckenbauer,mwenyekiti wa kamati ya maandalio ya kombe lililopita la dunia nchini Ujerumani lakini pia meneja wa timu ya Taifa ya Ujerumani Oliver Bierhoff:Ameionaje kura ya jana ?

“Tumeridhika na kura ilivyopigwa.Hatukuangukia kundi dhaifu,lakini ni Russia na Finland ni maadui tunaoweza kuwashinda.”

Ama katika kanda ya Afrika ya timu 48 zilizogawiwa makundi 12 ya timu nne-nne na kucheza kwa mfumo wa Ligi,washindi wa kila kundi na timu 8 bora kabisa zitakazomaliza nafasi ya pili zitaingia duru ya tatu.Katika duru hiyo ya 3 , timu za nchi 20 zitagawiwa makundi 5 ya timu nne-nne zitakazocheza pia kwa mfumo wa ligi-nyumbani na ugenini.Washindi 5 wa makundi hayo watakata tiketi 5 za Afrika kwa kombe la dunia 2010 nchini Afrika Kusini.Ikiwa Afrika Kusini itawasili duru hii ya tatu,pointi zake hazitahesabiwa katika kuania nafasi ya kombe la dunia ,kwani inaingia bila kupingwa.

Afrika kusini,mwenyeji, imeangukia kundi lenye adui mkali Nigeria, chini ya kocha mjerumani Berti Vogts.Timu nyengine kundi hili ni Guinea ya Ekweta na Sierra Leone.

Katika kundi jengine gumu la kanda ya Afrika, Senegal na Algeria wataumana katika kundi la 6 huku Liberia na Gambia zikijaza nafasi nyengine katika kundi hili.kundi la 12 linajumuisha Congo,Misri,Malawi na Djibouti.

Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo lakini, iko kundi la 10 pamoja na Mali,Chad na Sudan.

Tanzania –Taifa Stars wana kibarua kigumu mbele ya simba wa nyika-Kamerun.Nafasi yao ya kutamba mbele ya Cape Verde na Mauritius ni nzuri. ilivyopokewa Tanzania.

Harambee Stars-Kenya imeangukia kundi moja na Guinea,Namibia na Zimbabwe.Je, wakenya Kenya haikuwahi kushiriki katika finali za Kombe la dunia.

Wanariadha 2 maarufu jana walitunzwa zawadi za “wanariadha bora wa mwaka”:Bingwa wa dunia wa mita 100 wanaume, Ryson Gay na mwanariadha wa masafa ya kati na marefu wa Ethiopia M eseret Defar, walitunzwa jana katika tafrija maalumu ya shirikisho la riadha ulimwenguni-IAAF huko Monte Carlo.Defar aliweka rekodi ya maili 2 wakati wa mashindano ya Van Damme Memorial hapo Septemba 14 2007 na hivyo, ameivunja rekodi yake binafsi ya dunia kwa sek.12

Muamerika Tyson Gay alishinda mita 100 na 200 katika mashindano ya mwaka huu ya ubingwa wa riadha duniani huko Osaka,Japan.Alitunikiwa pia zawadi nyengine hapo kabla ile ya “Jesse Owens Award”.

 • Tarehe 26.11.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CTLI
 • Tarehe 26.11.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CTLI