1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya duru ijayo ya Champions League imepigwa:

18 Desemba 2009

Bayern Munich inacheza na Fiorentina wakati AC Milan yaikaribisha Manchester united.

https://p.dw.com/p/L7zS
Bastian Schweinsteiger, walipoikomea Juventus 4:1Picha: AP

Bayern Munich ikiteremka uwanjani leo (Ijumamosi)na jogoo lake la Ufaransa, Franck Ribery,inatumai viongozi wa Ligi -Bayer Leverkusen, watateleza na wao watatawazwa mabingwa wa taji la nusu-msimu.

Ndoto sawa na hiyo, wanayo Manchester United katika Premier League-Ligi ya Uingereza, ikitazamia viongozi wa Ligi Chelsea, hawatambi kesho (Ijumapili ) mbele ya Westham. Kura imepigwa kwa duru ya kwanza ya kutoana ya Champions League.Togo na Algeria, zatangaza vikosi vyao kwa Kombe lijalo la Afrika la mataifa mwezi ujao nchini Angola.

Stadi wa Bayern Munich,ambae amekuwa gurudumu la mashambulio yao usoni,mfaransa Franck Ribery, arejea leo uwanjani katika mpambano wa mwisho wa Bundesliga mwaka huu utakao mtawaza bingwa wa taji la nusu-msimu.Munich ilinadi kitambo kwamba, ifikapo X-masi, itakuwa kileleni mwa Bundesliga na leo inabidi kutimiza ndoto hiyo kivitendo.

Mahasimu wao ni Hertha Berlin, timu iliopo mkiani kabisa mwa ngazi ya Bundesliga na ambayo bila shaka, itachachamaa kuzuwia kuteremshwa ngazi na mapema huko Allianz Arena.

Ribery , ambae amekuwa katika shina la mjadala wa kuhamia Real Madrid,Spain, tangu majira ya kiangazi, amekataa hadi sasa, kusema iwapo atabakia Munich baada ya mwisho wa msimu huu au la.

Viongozi wa Ligi, Bayer Leverkusen , ambayo haikushindwa hadi sasa, inatumai kushinda leo nyumbani mbele ya Borussia Moenchengladbach, ambayo nayo pia imeshindwa mara 1 tu katika mechi 7 zilizopita . Schalke iliopo nafasi ya pili katika ngazi ya Bundesliga, ilikuwa jana wenyeji wa Mainz.

Mabingwa Wolfsburg, wanacheza na Eintracht Frankfurt wakati Hannover waikaribisha nyumbani Bochum. Stuttgart inacheza na Hoffenheim, ambayo imerefusha mkataba wa msenegal Demba Ba na mnigeria Chinedu Obasi.Stuttgart itapaswa basi kuchunga.

Jumapili (kesho) Hamburg, inaumana na jirani zao wa kaskazini Werder Bremen wakati changamoto ya kufa-kupona itakuwa kesho mjini Cologne ambako wenyeji FC Cologne wana miadi na Nuremberg.Wakati Nüremberg yataka kujikomboa mkiani mwa Ligi, FC Cologne, lazima itambe nyumbani, kwani ni kitambo kirefu haikutia bao wala kuondoka na pointi 3.

Ama katika Premier League-ligi ya Uingereza, ipi kati ya timu 4 ziliopo kileleni itatoroka msimu huu na taji la ubingwa, haijulikani:

Kocha wa Chelsea, viongozi wa Ligi,Carlo Ancelotti ameungama kwamba Chelsea, inahitaji kumtuliza shetani, ili kuhimili vishindo vya kinyan'ganyiro cha Ligi baada ya kuzabwa mabao 2-1 na Portsmouth. Chelsea iko pointi 3 usoni kabla ya mapambano wa kesho na West ham United. Mahasimu wao Manchester united wana miadi na Fulham.Arsenal iko nyumbani ikiikaribisha mikono miwili Hull City. Liverpool inacheza na Portsmouth.Aston villa yakumbana na Stoke City. Manchester City inakumbana na Sunderland.Jumatatu Wigan Athletic itaikaribisha nyumbani Bolton Wanderes.

Kura imepigwa (Ijumaa) kwa duru ya kwanza ya kutoana ya kuania Kombe la Champions League-Kombe la klabu bingwa barani Ulaya msimu huu:

VFB Stuttgart ,itacheza na mabingwa FC Barcelona; Bayern Munich itaikaribisha nyumbani Fiorentina; Inter Milan inacheza na Chelsea,Olympique Lyon itaumana na Real Madrid.CSKA Moscow itacheza na Sevilla wakati Olympiakos Piraeus, itabidi kujiwinda kupambana na Girondins Bordeaux. FC Porto maadui zao watakuwa Arsenal wakati Manchester United watapambana na AC Milan.

Firimbi italia mwezi ujao kwa Kombe la Afrika la Mataifa , nchini Angola, jirani na mwenyeji wa Kombe la dunia 2010 Afrika Kusini: Timu 16 bila ya Afrika Kusini, zitakuwa uwanjani. Algeria na Togo, zimesha tangaza listi ya timu zao: Katika kikosi cha Togo, yuko mlinzi wa viongozi wa Bundesliga-Bayer Leverkusen, Assimiou Toure, na usoni yumo mshambulizi Emmanuel Adebayor, anaetamba katika Premier League.

Kikosi cha Algeria, ambayo kinyume na Togo , ni mojawapo ya timu 6 za Afrika katika Kombe la dunia 2010, Chadli Amri wa Mainz na Karim Matmour wa Borussia Moenchengladbach pamoja na Yacine Bezzaz wa Strassbourg ya Ufaransa. Kombe la Afrika la Mataifa ,Januari ijayo linafungua pazia la Kombe la dunia Afrika Kusini hapo Juni 11.2010.

Mwandishi: Ramadhan Ali /RTRE

Uhariri: Aboubakar Liongo