1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la G20 latimiza miaka 10

14 Desemba 2009

Kundi la mataifa 20 yaliyostawi kiviwanda kote ulimwenguni yakiwemo yanayoinukia limetimiza miaka 10 tangu kuasisiwa kwake

https://p.dw.com/p/L1wF
Viongozi wa kundi la G20Picha: AP

Viongozi wa kundi hilo walikutana kwa mara ya kwanza mjini Berlin tarehe 15 na 16 mwezi wa Disemba mwaka 1999.Lengo la kuliunda kundi hilo lilikuwa kuuimarisha uchumi kufuatia mtikisiko wa fedha ulioliathiri bara la Asia mwaka 1997.Hata hivyo kundi hilo lilishindwa kuuzuwia mtikisiko wa kiuchumi uliotokea jambo ambalo ni la ajabu katika historia ya kundi la G20

Kundi la G20 lilianzishwa kwa madhumuni ya kuyaleta pamoja mataifa yanayoinukia na yale yaliyostawi kiviwanda.Azma yao hasa ilikuwa kujadiliana pamoja kuhusu masuala muhimu ya kiuchumi na fedha katika ngazi za kimataifa.Katika kikao cha masuala ya Uchumi kilichofanyika mjini Cologne mwezi wa Juni mwaka 1999 kulitolewa pendekezo jipya.Mawaziri wa Fedha pamoja na magavana wa mabenki ya mataifa yaliyostawi kiviwanda na yanayoinukia waliafikiana kuwa na vikao vya kila mara kulijadili suala hilo.Baada ya miezi michache,katika mwezi wa Disemba,kikao cha kwanza cha kundi la G20 kilifanyika mjini Berlin. Dirk Messner ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Ujerumani ya maendeleo,alisema

''Mataifa yanayoinukia na yanayoendelea yalikuwa hayajakuwa na mpangilio maalum,lilikuwa kundi kubwa ambalo halina ushawishi mkubwa.Kundi la G20 lilikuwa jaribio la mataifa yanayoinukia kuyaimarisha masuala ya uchumi pamoja na uwezo wao kisiasa kusababisha tofauti katika ngazi ya kimataifa.''

Kundi hilo hilo la G20 linawaleta pamoja wawakilishi wa mawaziri wa fedha na magavana wa mataifa 19.Kati yao ni mataifa tajiri ya kundi la G7 ambayo ni Ujerumani,Ufaransa,Uingereza,Italia,Japan,Canada na Marekani.Kundi hilo pia linayaleta pamoja mataifa wanachama wa kundi la G8 ikiwemo Urusi pamoja na Argentina,Australia,Brasil,China,India,Indonesia,Korea Kusini,Mexiko,Saudi Arabia,Afrika Kusini na Uturuki.

G8 Gipfel in L`Aquila, Italien: G8- und G5-Regierungschefs
Viongozi wa kundi la G8Picha: AP

Mwanachama wa kujitegemea wa 20 ni Umoja wa Ulaya unaowakilishwa na kiongozi wa kamisheni ya Umoja huo pamoja na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Ulimwenguni IMF.

Kundi hilo la mataifa 20 yaliyostawi kiviwanda na yale yanayoinukia linachangia katika asili mia 90 ya pato la kimataifa kote ulimwenguni,asili mia 80 ya biashara ya ulimwengu na thuluthi mbili ya wakaazi wote ulimwenguni wote wakishiriakana na kuwa na lengo moja. Dirk Messner wa taasisi ya maendeleo ya Ujerumani anafafanua umuhimu wa mataifa yanayoinukia,''Kiasi cha miaka 15,16 au 17 hivi wakati masuala ya kisoshalisti yalipokuwa yanaanza kuupoteza umuhimu wake,China ilikuwa mshirika mdogo kiuchumi .Kwa sasa hilo limebadilika kwani mchango wa China katika uchumi wa Ulimwengu ni mkubwa katika uwekezaji wa moja wa moja.India ni taifa ambalo lilijiunga na mkumbo huu baadaye kidogo hususan katika masuala ya uchumi ila kwa sasa ni taifa muhimu.Kutokana na hilo kundi la G20 halina budi ila kuubadili mtazamo wake kwani kumekuwa na madabiliko yanayowakilisha uzito wa nchi.''

Kabla ya kutimiza miaka 9 tangu kuasisiwa kwake ulimwenguni ulikabiliwa na mtikisiko wa kiuchumi baada ya benki ya Lehman Brothers ya Marekani kufilisika.Kundi hilo lilikabiliwa na kibarua kipya sasa cha kuubadili mwelekeo wake hususan kwenye masoko ya fedha ya kimataifa.Kulingana na Dirk Messner wa taasisi ya maendeleo ya Ujerumani kundi hilo halina budi ila kuupanua wigo wake,''Kwa sasa ajenda ya kundi imebadilika na majukumu yameongezeka kwani baada ya mtikisiko wa kiuchumi kutoka kundi la G8 linalazimika kuchukua nafasi nyengine.Kundi la G8 linaloyaleta pamoja mataifa tajiri lina kibarua cha maandalizi ya mikutano yote ya G20 itakayoyajadili masuala ya uchumi ya ulimwengu pamoja na siasa.Ajenda ya G20 kwa sasa inajumuisha masuala ya hali ya hewa,umasikini,uhamiaji na sera za kimataifa.

Miaka 10 baada ya kuasisiwa kwake kundi la G20 limeimarika ukililinganisha na lile la G8 linaloyaleta pamoja mataifa nane tajiri ulimwenguni.Kundi la G8 lilikuwa linauongoza ulimwengu mzima ila kulikuwa na haja ya kuyajumuisha mataifa yanayoinukia.Kwa sasa mataifa hayo yanayoinukia yamekuwa sehemu ya kundi la G20 na pia kuna wazo la kuyajumuisha mengine ambayo si ya kundi hilo ili kuunda kundi la G172.

Mwandishi:Thelma Mwadzaya-ZPR/Klaus Ulrich

Mhariri:Abdul-Rahman