1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kujiuzulu kwa Rais wa Banki ya Dunia

Ramadhan Ali18 Mei 2007

Rais wa Banki Kuu ya Dunia Wolfowitz ametangaza kujiuzulu Juni 30 ya mwezi ujao.Anaitikia shinikizo kali alilotiwa wiki chache zilizopita.

https://p.dw.com/p/CB44
Paul Wolfowitz
Paul WolfowitzPicha: AP

Baada ya mabishano ya wiki kadhaa,rais wa Banki kuu ya Dunia,Paul Wolfowitz alitangaza jana kuwa anajiuzulu.Tume ya uchunguzi ya Banki kuu hiyo ilimkuta Bw.Wolfowitz amekwenda kinyume na kanuni za Banki hiyo alipompandishia mshahara na kumpandisha cheo rafiki yake wa kike.

Wolfowitz,makamo waziri wa ulinzi wa zamani,ametangaza mwishoe, kuwa atan’gatuka madarakani Juni 30.

Msemaji wa ikulu ya Marekani Tony Fratto amemueleza Wolfowitz ni mtu mwema ambae anahurumia sana maafa yanayowapata masikini ulimwenguni.Ikulu ya Marekani ,alisema, ingeliona bora angebakia madarakani kama rais wa banki Kuu ya Dunia,lakini rais Bush shingo upande amebidi kuridhia uamuzi wake wa kujiuzulu-alisema Tony Fratto.

Nae waziri wa fedha wa Marekani HENRY PAULSON alinukuliwa kusema,
”Ninakusudia kuchukua hatua haraka kumsaidia rais kumteua mtu mwengine kuiongoza Banki kuu ya Dunia .Nitashauriana na wenzangu ulimwenguni katika kumsaka kiongozi mpya atakaendeleza kazi ya kutoa nafasi kwa masikini kabisa ulimwenguni kwa kuhakikisha fedha zinatumiwa barabara kugharimia miradi ilio-mizuri.” Mwisho wa kumnukulu.

Nae Seneta CHRISTOPHER DODD, anaegombea kiti cha urais kwa niaba ya chama cha Upinzani cha Democratic party alieleza kuwa vitendo vya Bw.Wolfowitz viliweka pingamizi kwa Banki Kuu ya dunia kutekeleza jukumu lake kubwa la kuondosha umasikini duniani.Kujiuzulu kwake, aliongeza, kutasaidia kurejesha heshima na uaminifu wa Banki Kuu ya Dunia.

Dr.Eckhard Deutscher, mjumbe huyo wa Ujerumani,yalibainisha dhahiri-shahiri kuwa bodi ya Banki kuu imeona kuwa Bw.Wolfowitz hangeweza tena kuongoza barabara shughuli za Banki Kuu ya Dunia baada ya yaliotokea:

“Sababu zilizoongoza serikali ya Ujerumani kumuona Bw.Wolfowitz hakubaliki tena zinatokana na jinsi alivbyokua akiongoza Banki kuu ya dunia.Hasa alikiuka maadili na kanuni zinazowahusu watumishi na jinsi pia alivyoukabili mzozo wa hivi punde.”

Bw.Deutscher,akaongeza kwamba tangu watumishi wa Banki kuu ya Dunia hata uongozi wa banki hiyo pamoja pia na nchi zenye hisa zao kwenye Banki hiyo ,hawakuwa tena na imani na uongozi wa Bw.Wolfowitz.

Kwa muujibu wa mkataba wake,Bw.Wolfowitz,kwa kun’gatuka madarakani kabla ya wakati, ataondoka na mshahara wa mwaka mzima wa dala 375.000.zaidi ya hapo ameeleza mjumbe wa Ujerumani Bw.Deutscher,hakuna ahadi zaidi za marupurupu alizoahidiwa.

Siku za usoni za rafiki wa kike wa Bw.Wolfowitz,si swala lililojadiliwa kabisa na bodi hiyo.

Kwa desturi,marekani imekuwa ikiteua nani awe rais wa banki kuu ya dunia.Iwapo desturi hii sasa iendelezwe au la,kuna sauti nyingi zinazodai ikome.

Mjumbe wa Ujerumani asema: “Mwaka 2004 tulipitisha azimio katika halmashauri kuu kuwa kila mkurugenzi-tendaji aweza kumpendekeza mtetezi wa wadhifa huo.Kwahivyo ,sio lazima kutoka ndani ya banki Kuu au bodi yake wadhifa wa urais moja kwa moja uende kwa Mmarekani.Kila mmoja ana haki kutoa pendekezo.Hata nchi zilizoinukia na nchi changa zaweza kumtoa rais.”

Bw.Wolfowitz, anabakia madarakani hadi mwisho wa mwezi ujao-Juni 30.Leo hii, Halmashauri kuu ya Banki Kuu ya dunia, inakutana kuamua hatua gani zichukuliwe wiki zinazokuja.