1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuitisha mapema uchaguzi ni mbinu ya kisiasa

P.Martin - (RTRE)2 Machi 2009

Mgombea urais nchini Afghanistan amemkosoa Rais Hamid Karzai alieamua kuitisha uchaguzi mwezi wa Aprili badala ya Agosti tarehe iliyopangwa hapo awali.Anasema,wagombea wengine hawatokuwa na nafasi ya kufanya kampeni.

https://p.dw.com/p/H4BY
Afghan President Hamid Karzai gestures during a press conference at the presidential palace in Kabul, Afghanistan, Sunday, June 15, 2008. Karzai has issued a forceful warning to militants in Pakistan, saying he will send Afghan troops across the border to combat Taliban insurgents. (AP Photo/Rahmat Gul)
Rais wa Afghanistan,Hamid Karzai.Picha: AP

Kwa maoni ya wachambuzi wa kisiasa,amri ya Rais Hamid Karzai kuitisha uchaguzi mapema hivyo ni mbinu ya kisiasa kutaka kulazimisha makundi ya upinzani kumuachilia madarakani pale muhula wake utakapomalizika kikatiba mwisho wa mwezi Mei.Amri ya Karzai inatumbukiza demokrasia changa ya Afghanistan katika hali mpya ya kikatiba na kusababisha mvutano na tume ya uchaguzi iliyopanga kufanya uchaguzi huo tarehe 20 mwezi wa Agosti. Hata Marekani,mshirika wa Karzai iliunga mkono tarehe hiyo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Robert Wood amesema, Marekani inaelewa sababu za msingi zilizoelezwa na Karzai, lakini inaamini kuwa mwezi wa Agosti ungekuwa wakati bora zaidi kufanya uchaguzi katika mazingira ya usalama.Kwani Rais wa Marekani Barack Obama ametoa amri ya kupeleka wanajeshi 17,000 ziada nchini Afghanistan kuimarisha usalama wakati wa uchaguzi mwezi wa Agosti, ikihofiwa kuwa wanamgambo wa Taliban watazidisha mashambulio yao.Kwa kuitisha mapema uchaguzi,vikosi havipewi wakati wa kutosha kufika Afghanistan.

Vile vile,wagombea wengine hawatokuwa na wakati wa kutosha kufanya kampeni ya uchaguzi analalamika mgombea urais Ashraf Ghani Ahmadzai. Amesema,wao walikuwa wakijitayarisha kwa uchaguzi wa Agosti lakini uamuzi huo wa ghafula kuitisha uchaguzi mapema utasababisha matatizo fulani.Wakati huo huo,tume huru ya uchaguzi inasema,uchaguzi hauwezi kufanywa wakati wa majira ya baridi kali nchini Afghanistan kwani itakuwa vigumu kufikia maeneo mengi kwa sababu ya barafu na hivyo wakaazi wa maeneo hayo watanyimwa haki ya kupiga kura.

Kiongozi wa chama kimojawapo kikuu cha upanzani Hafiz Mansur anasema, chama chake kina imani na katiba lakini isitumiwe kusababisha vurugu na machafuko na kufanyika uchaguzi usio wa haki.Amri ya Karzai inasema, uchaguzi ufanywe kuambatana na katiba-yaani muhula wake unamalizika tarehe 21 mwezi wa Mei na uchaguzi wa kumchagua mrithi wake unapaswa kufanywa kati ya siku 30 na 60 kabla ya tarehe hiyo-kwa hivyo siku ya mwisho kabisa kwa uchaguzi huo kuweza kufanyika ni Aprili 21.

Kwa upande mwingine sheria ya uchaguzi inasema, uwepo angalao muda wa siku 120 kutayarisha uchaguzi-hiyo humaanisha muda uliopo hautoshi kwa uchaguzi kufanyika mwezi wa Aprili.Mgombea urais Ashraf Ghani Ahmadzai ametoa mwito wa kufanywa mkutano mkuu wa viongozi wa kisiasa nchini Afghanistan kuamua njia bora kabisa ya kuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki.

Amri ya Karzai inasema,uchaguzi ufanywe kuambatana na katiba-yaani muhula wake unamalizika tarehe 21 mwezi wa Mei na uchaguzi wa kumchagua mrithi wake unapaswa kufanywa kati ya siku 30 na 60 kabla ya tarehe hiyo-kwa hivyo siku ya mwisho kabisa kwa uchaguzi huo kuweza kufanyika ni Aprili 21.Kwa upande mwingine sheria ya uchaguzi inasema, uwepo angalao muda wa siku 120 kutayarisha uchaguzi-hiyo humaanisha muda uliopo hautoshi kwa uchaguzi kufanyika mwezi wa Aprili.