1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari lamalizika

Mohammed Khelef15 Juni 2016

Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari linaloandaliwa kila mwaka na Deustche Welle limemalizika kwa wito kwa waandishi wa habari kutumia taaluma zao kuyaelezea madhila ya majanga ya kimaumbile na ya kibinaadamu.

https://p.dw.com/p/1J75c
Mkurugenzi Mkuu wa DW, Peter Limbourg, akihitimisha siku tatu za Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari mjini Bonn siku ya Jumatano ya Juni 15, 2016.
Mkurugenzi Mkuu wa DW, Peter Limbourg, akihitimisha siku tatu za Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari mjini Bonn siku ya Jumatano ya Juni 15, 2016.Picha: DW/K. Danetzki

Kongamano lilimalizika kwa mkurugenzi mkuu wa Deutsche Welle, Peter Limbourg, kuwashukuru washiriki kwa moyo mkubwa wa kujitolea ndani ya siku tatu za kukusanyika katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Bonn.

"Nawashukuruni nyote muliochangia kongamano hili la kilimwengu juu ya vyombo vya habari, kwa michango, mawazo, kazi, na kwa pesa zenu pia. Nawashukuru wafadhili na washirika wetu. Na shukurani kwa watu walioyaandaa yote haya."

Hii ilikuwa alama ya kuhitimisha rasmi siku tatu za mijadala na mikutano iliyofanyika kwenye vikao 65 vya kongamano la mwaka huu, chini ya maudhui kuu ya "Vyombo vya Habari, Uhuru na Maadili."

Hata hivyo, Limbourg aliwaambia washiriki hao kuwa si wao pekee waliokuja kujifunza, bali hata wenyeji wamefaidika na mawazo yaliyotoka kwa wageni wao, hata kama mengine yanabeba ukweli mchungu.

"Jambo muhimu zaidi ni kuwa sio tu tumezungumzia maadili na kusema kuwa tutazameni jinsi Ulaya tulivyo na kiwango cha juu cha maadili, bali pia tumeingia kwenye mjadala nanyi na mukatukumbusha kuwa sisi watu wa Ulaya baadhi ya wakati hatuheshimu maadili hayo, kwa mfano kama munaposema tunawauzia silaha watawala madikteta, tunachafua mazingira na pia kushirikiana na serikali za kifisadi."

Ujumbe wa mabadiliko ya tabia nchi

Pamoja na salamu hizo za kushukuru na kuaga, jukwaa kuu katika siku hii ya mwisho lilikuwa ni la Mkuu wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabia Nchi Ulimwenguni, Christiana Figeueres.

Mkuu wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabia Nchi, Christiana Figueres, akizungumza na washiriki wa Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari mjini Bonn siku ya Jumatano ya Juni 15, 2016.
Mkuu wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabia Nchi, Christiana Figueres, akizungumza na washiriki wa Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari mjini Bonn siku ya Jumatano ya Juni 15, 2016.Picha: DW/K. Danetzki

Mkuu huyo aliwakumbusha waandishi wa habari jukumu kubwa walilonalo katika kuuelezea na kuuchambua ukweli wa kitisho kinachoikabili sayari ya dunia kutokana na majanga ya kimaumbile na yale ya kibinaadamu.

"Kuna jambo moja lenye maslahi kwa wanaadamu wote kwa pamoja, bila ya kujali ulipozaliwa, dini yako, jinsia yako au umri wako. Sote tuna jambo moja lenye maslahi kwetu sote, nalo ni amani na utulivu. Na sasa tuna fursa ya kuyafanya maslahi haya yadumu kwa kuzitumia nyenzo ambazo zimekubaliwa na serikali na mashirika yote duniani."

Kwa kutaja nyenzo hapa, Figueres alikuwa anamaanisha makubaliano ya Paris ya Disemba 2015, ambayo yalifunguwa njia ya maridhiano ya kilimwengu juu ya ulinzi wa tabaka hewa na kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, watu wapatao milioni 65 watalazimika kuyakimbia makaazi yao ndani ya miongo miwili ijayo kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Kongamano la mwaka huu lilitawaliwa kwa kiasi kikubwa na mijadala juu ya matumizi ya mitandao ya kijamii, nafasi yake na mchango wake katika mageuzi ya kisiasa na kijamii, biashara, na namna udhibiti wake unavyotafsiri maadili na uhuru wa kujieleza.

Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Iddi Ssessanga