1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la vijana la Afrika laingia nusu-finali.

26 Januari 2009

Nigeria,Ghana,Kamerun na Afrika Kusini zaingia nusu-finali.

https://p.dw.com/p/GgZ9
Adebayo-jogoo la ArsenalPicha: picture-alliance/dpa

Katika kinyanganyiro cha kombe la Afrika la vijana mjini Kigali,Nigeria na Afrika Kusini, zimeingia nusu-finali ya kwanza wakati Simba wa nyika- Kamerun na Black Stars (Ghana) wanacheza ile ya pili-finali jumapili ijayo.

Je, Young Africans ya Tanzania imeshalitia taji mfukoni kabla msimu kumalizika ?

Steven Gerrad aikoa tena Liverpool aliposawazisha bao 1:1 na Everton katika kinyanganyiro cha kombe la FA.

Katika kinyanganyiro cha Kombe la Afrika la vijana chini ya umri wa miaka 20 mjini Kigali,Ruanda timu 4 zimekata tiketi zao kwa duru ya nusu-finali jumatano hii: Ghana na Kamerun kwa upande mmoja na Nigeria na Afrika Kusini.Nigeria, tayari imetawazwa mara 5 mabingwa wa Kombe hili na pamoja na Ghana, timu zao chipukizi zimeshatamba katika kombe la duinia la FIFA ambalo mwaka huu litaaniwa Misri.

Ivory Coast na Mali tayari zimeshapigwa kumbo.

Huko Tanzania, Ligi ya Tanzania-bara inaendelea huku mabingwa young Africans nao wakiendelea kutamba kabla ya miadi yao ya kombe la klabu bingwa barani Afrika na mabingwa wa visiwa vya Comoro mjini Dar-es-salaam mwishoni mwa wiki ijayo.

Simba mahasimu wao wa jadi wameangukia nafasi ya 5 na ni vigumu kunguruma alao msimu huu.

Katika medani ya dimba huku Ulaya, Premier League-Ligi ya Uingereza ilipumzika mwishoni mwa wiki na kuuacha uwanja kwa kombe la FA-kombe la shirikisho la dimba la Uingereza.

Jane Nyingi anawachukua viwanjani:

Nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard kwa mara nyengine aliliokoa jahazi lake lisizame lilipoenda jana mrama.Katika duru ya 4 ya kombe la FA, Gerrad alitia bao kusawazisha 1:1 na Everton.

Gerrad alilifumania lango la Everton dakika 9 baada ya kipindi cha mapumziko na hivyo, kufuta bao la Joleon Lescott alilotia katika kipindi cha kwanza.

Hapo kabla hapo jana, makamo-bingwa wa mwaka uliopita wa Kombe la FA Cardiff City, waliwabana mabingwa mara 10 wa kombe hili Arsenal na kuachana nao sare 0:0.

Arsenal kwa kweli, ilishika usukani wa changamoto yao katika kipindi cha pili ,lakini licha ya kudhibiti mchezo,majogoo wao hawakuwika.Na walipokaribia kupiga hodi , kipa wa Cardiff, Peter Enckelmann aliwakatisha tamaa.

washindi wa duru ya pili ya mpambano huu kati ya Arsenal na Cardiff ataweka miadi na West Bromwioch Albion au Burnley.

Mabingwa wa kombe la FA Portsmouth jumamosi walipigwa kumbo na timu ya daraja ya pili ya Swansea kwa mabao 2:0.

Manchester united ilitoka nyuma na kuiambia Tottenham Hotspurs kutangulia si kufika.Manu ikatoroka na ushindi wa mabao 2-1 na sasa imeingia katika duru ya timu 16 zilizosalia katika kinyanganyiro cha Kombe hili la FA. Manu itaweka miadi ama na Nottingham forest au Derby County duru ijayo.

Upande wapili wa mpaka huko Ufaransa, Kombe la shirikisho la dimba pia lilianiwa: Paris st.Germain ilitamba kwa mabao 3:0 mbele ya Ajaccio.Le Havre ilikandikwa bao 1:0 na Le Mans. Stade rennes iliiitoa St.Etienne kwa mabao 2: 0.

Uhispania ilikua na kalenda ya kawaida ya kinyanganyiro cha ubingwa:

Viongozi wa Ligi-FC Barcelona, waliirarua Numancia kwa mabao 4-1 wakati Villareal ilimudu suluhu tu ya bao 1:1 na Osasuna hapo Jumamosi. Getafe iliikun´guta jana Sporting Gijon mbaoa 5-1 wakati Malaga ilitoka suluhu na Atletico Madrid ya bao 1:1.

Real Mallorca (Mayoka) ilitamba kwa mabao 3-1 mbele ya Valencia.Mkamerun Samuel Eto-o anaendelea kuongoza orodha ya watiaji magoli katika La Liga-Ligi ya Uhispania.Ameshatia mabao 19 akifuatwa na David Villa wa Valencia.

Ama katika changamoto za Seriea A-Ligi ya Itali,AC Milan ilitamba kwa mabao 4-1 la Bologna wakati mahasimu wao wa mtaani Inter Milan waliitoa Sampdoria kwa bao 1:0.AS Roma ilinguruma kwa mabao 3:0 mbele ya Napoli .Inter inaendelea kuongoza Ligi ya Itali.