1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Klabu ya tabaka la juu?

4 Juni 2007

Ni siku mbili tu zilizosalia hadi mkutano wa kilele wa nchi nane zilizostawi kiviwanda duniani, G8, utakapoanza mjini Heiligendamm, Ujerumani. Yaliyoonekana katika siku zilizopita lakini ni upande mwingine wa mkutano huo, yaani ghasia zilizotokea mjini Rostock, karibu na Heiligendamm, pale wanaharakati wanaopinga sera za utandawazi waliandamana. Watu karibu ya 1000 walijeruhiwa. Katika uchambuzi wake, mwandishi wetu Peter Philipp anachuguza ukosoaji na umuhimu wa mkutano wa G8.

https://p.dw.com/p/CHDG

Matumizi ya nguvu hayawezi kustahamiliwa, wala haiwezekani kutumia nguvu badala ya hoja. Hilo linakubaliwa na wote, wakiwa ni wapinzani wa utandawazi au wale wanaounga mkono sera hizo za kimataifa. Wale waliotumia nguvu na kuanzisha fujo hizo waliwaathiri wale wanaotaka kueleza wasiwasi wao juu ya sera za nchi hizo za G8. Kuanzia sasa, ukosoaji huenda utafahamika kuwa ni matumizi ya nguvu.

Lakini hii haiwezekani, kwani ukosoaji huu unafaa, hata baada ya ghasia zilizotokea Rostock. Lakini ukosoaji huu usiwe tu kulaumu juu ya gharama kubwa ya utaratibu wa kuhakikisha usalama wa washirika, yaani hasa gharama za ujenzi wa seny'enge zinazozunguka pahala pa mkutano na vikosi vya polisi vilivyoletwa kulinda usalama. Lakini hizo zi ishara tu ya maendeleo ambayo yalianza zamani:

Wakati viongozi wa nchi zinazoongoza kiviwanda duniani walipoanza kukutana mara kwa mara, mikutano yao ilikuwa isiyo rasmi. Malengo yalikuwa zaidi kukutana ana kwa ana, kuzungumzia wazi mawazo na sera zao, yaani mbali na kamera na vyombo vya kunasia sauti. Lakini siku hizo za mazungumzo ya kibinfasi zimeshapitwa na wakati. Leo mikutano ya viongozi wa G8 ina ratiba maalum na lengo ni kutafuta suluhisho kwa shida za ulimwengu.

Hilo ndilo lakini tatizo la kundi la G8: Yaani ni nchi zinazotaka kutatua matatizo ambayo ziliyasababisha zenyewe. Mfano mmoja ni matatizo ya bara la Afrika, jengine ni suala la hali ya hewa. Orodha ni ndefu. Mataifa ambayo yalikuwa na mamlaka ya ukoloni, au mengine ambayo hata bila ya historia ya kikoloni yanazitumia nchi za Kiafrika kama watoaji wa mali ghafi tu, sasa yanaanzisha miradi mipya ya msaada kwa bara la Afrika. Pia ni mataifa yanayochafua zaidi mazingira ambayo sana yanajaribu kuzungumzia kulinda hali ya hewa. Kimsingi, si kitu kibaya. Lakini, kama tumeshawahi kuona mara nyingi, maneno yao hayafuatiwa na hatua. Kwa hivyo matumaini kabla ya mkutano wa Heiligendamm ni madogo.

Wale ambao wanaandaa miradi mikubwa kule Heiligendamm wanaonekana wameshasahau makosa yao, na badala yake wanajitambulisha kama klabu ya tabaka la juu ambayo ina usemi mkubwa katika dunia hii. Dunia lakini imebadilika tangu mkutano wa kwanza wa nchi za kundi la G8. Siku hizi China na India pia ni nchi kubwa za kiviwanda, lakini hazikuingizwa katika klabu ya G8 bali hualikwa kama wageni tu. Ni kama klabu hii haitabadilishwa tena, kama baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Huo ni mfano mzuri wa tabia za kujivuna na kulinda mamlaka yao. Sen'yenge kubwa za Heiligendamm zinaimarisha tu picha hiyo.

Hoja nyingine ni kwamba, ikiwa nchi za G8 zitaongezwa kuziingiza nchi nyingine za kiviwanda, basi mikutano yao itachukua nafasi na jukumu la Umoja wa Mataifa. Ni kweli kabisa. Kwa hiyo inabidi masuala yanayozungumziwa na G8 yawekwe mbele ya hadhara kuu ya Umoja huo. Kwani ni masuala ambayo lazima yatatuliwe na watu wote kwa pamoja, si tu na klabu maalum.