Kituo cha televisheni ya taifa chashambuliwa Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.08.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kituo cha televisheni ya taifa chashambuliwa Syria

Mripuko wa bomu umetokea katika jengo la makao makuu ya televisheni ya taifa ya Syria, yaliyopo mjini Damascus. Waziri wa habari wa Syria amesema watu kadhaa wamejeruhiwa lakini hakuna aliyeuwawa.

Kituoc cha televisheni ya taifa Syria

Kituoc cha televisheni ya taifa Syria

Bomu hilo liliripuka katika ghorofa ya tatu ya jengo la televisheni ya taifa la Syria. Hata hivyo, kituo hicho kiliendelea kurusha matangazo yake na kumfanyia mahojiano waziri wa habari al-Zoabi aliyeeleza kuwa baadhi ya wafanyakazi wa kituo hicho walijeruhiwa na kuongezea kwamba pametokea uharibifu mkubwa. Hata hivyo, kituo hicho kiliweza kuendelea kurusha matangazo yake kwa sababu ya kuwa na studio na vifaa vya kutosha ambavyo havikuharibiwa.

Tarehe 27 Juni mwaka huu, kituo cha televisheni kiitwacho Al-Ikhbariya nacho kilishambuliwa kwa mabomu na risasi. Waandishi wa habari watatu pamoja na maafisa wa usalama wanne waliuwawa katika shambulio hilo. Waziri wa habari al-Zoani amesema hii ni ishara kwamba vituo vya televisheni vya Syria vinashambuliwa kwa sababu ya ujasiri wake, lakini hakuna kitakachoweza kuizuia sauti ya Syria.

Mapigano yaendelea Aleppo

Mapigano yaendelea Aleppo na kwengineko

Mapigano yaendelea Aleppo na kwengineko

Wakati huo huo, mapigano yameripotiwa katika baadhi ya maeneo ya mji wa Aleppo ulioko kaskazini mwa Syria. Shirika la kutetea haki za binadamu la Syria, lenye makao yake makuu London, Uingereza, limeeleza kwamba mapigano kati ya waasi na jeshi la Assad yalisababisha kifo cha kamanda mmoja wa waasi katika wilaya ya Salaheddin inayoshikiliwa na waasi kwa sasa. Majeshi ya Assad nayo yalimuuwa kwa risasi raia mmoja aliyekuwa akiwasaisdia watu waliojeruhiwa. Jumla ya watu 9 wameuwawa Aleppo leo, wanane kati yao wakiwa raia wa kawaida. Idadi ya waliouwawa leo asubuhi katika nchi zima ya Syria ni watu 19. Jana iliripotiwa kwamba watu 131 waliuwawa katika mapigano yanayoendelea nchi nzima. Hata hivyo, ni vigumu kuthibitsha idadi hiyo na Umoja wa Mataifa umeacha kuhesabau idadi ya watu wanaouwawa

Wapinzani wa utawala wa Assad wanaoishi uhamishoni wameishutumu serikali ya Syria kwa kuwauwa watu 40 katika mji mmoja uliopo kwenye eneo la kati la Syria. Kwa mujibu wa baraza la kitaifa la Syria, watu wapatao 120 walijeruhiwa katika mji wa Harbnafsa uliopo mkoani ya Hama. Baraza hilo linaeleza kuwa vikosi vya Assad viliingia kwa nguvu kwenye mji huo vikiwa na silaha nzito na kuushambulia kwa muda wa saa tano. Baraza la kitaifa la Syria linaliona shambulio hilo kama hatua ya serikali kuwatishia watu ili wayakimbie makaazi yao. Msemaji mmoja wa baraza hilo pia ameeleza kuwa Qatar na Saudi Arabia zinawapa waasi silaha, lakini silaha hizo hazitoshi kupambana kikamilifu na jeshi la Assad.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp/Reuters

Mhariri: Othman Miraji

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com