1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kisa cha kutekwa nyara watalii nchini Misri

Hamidou, Oumilkher24 Septemba 2008

Vikosi vya Sudan vinalizingira eneo la jangwani la Jebel Ouenet

https://p.dw.com/p/FOJH
Eneo la jangwani wanakoshikiliwa mahabusi wa nchi za magharibi pamoja na wenzao wa MisriPicha: picture-alliance/ ZB



 Vikosi vya Sudan vinalizingira eneo wanakoshikiliwa mahabusi 19,wakiwemo watalii 11 wa kizungu,katika jangwa la Sahara,karibu na mpaka wa Sudan na Misri.


Waziri wa utalii wa Misri,Zoheir Garanna ameliambia shirika la habari la Ufaransa hii leo,juhudi za kuwakomboa mahabusi hao zinaendelea, kwa siku ya tano tangu walipotekwa nyara.


Watalii kumi na mmoja,wakiwemo wajerumani watano,wataliana watano na  bibi mmoja wa kutoka Rumania,pamoja na wasaidizi wao sabaa wa kutoka Misri na mkuu wa shirika la Safari za utalii wametekwa nyara tangu ijumaa iliyopita .


"Wameonekana katika eneo la jangwani la Jebel Ouenat,kilomita 25 toka  mpaka wa Misri.Vikosi vya Sudan vinalizingira eneo hilo." Amesema hayo mkurugenzi wa itifaki katika wizara ya mambo ya nchi za nje aliyebainisha tunanukuu: "vikosi hivyo havina dhamiri ya kulivamia eneo hilo wasije wakayatia hatarini maisha ya mahabusi."Mwisho wa kumnukuu.


Baada ya patashika ya jumatatu kuhusu kuachiwa huru kwa uwongo mahabusi hao,viongozi wa serikali mjini Cairo wameamua kutotoa maelezo mengi kuhusiana na kisa hicho.


"Bora tusilizungumzie suala hili kabla ya juhudi za kuwakomboa mahabusi hazijafanikiwa"-amesema msemaji wa ikulu ya rais Suleiman Awadh.


Mawasiliano pamoja na wateka nyara yanaendelezwa kwa simu kati ya mkuu wa shirika la safari za watalii ambae ni miongoni mwa mahabusi,na mkewe Kirsten Butterweck-Abdel Rahim mwenye asili ya kijerumani.


Habari zinatofautiana kuhusu asili ya maharamia hao.Waziri wa utalii wa Misri Zuheir Garana amekanusha ripoti zinazosema maharamia hao ni raia wa misri.Vyombo vya habari vya Misri vinasema huenda wahalifu hao ni raia wa Tchad.


Eneo hilo la jangwani Jebel  Ouenat haliko mbali na Sudan na kutoka hapo kuna njia za vichakani pia za kuingia Libya na Tchad.


Kuna uvumi maharamia hao wanadai walipwe fedha kabla ya kuwaachia huru mahabusi .Ferdha hizo zinaanzia dala milioni nne hadi dala milioni sitini.


"Sasa wamepunguza kutoka dala milioni 60,hadi dala milioni kumi" duru za usalama zinasema.


Waziri wa utalii wa Misri alizitaja ripoti za vyombo vya habari kuhusu malipo ya dala milioni 6,milioni nane au hata milioni 15 kua "hazina msingi."