1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya afuta maandamano yaliyopangwa kufanyika kesho.

Halima Nyanza7 Januari 2008

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga amefuta maandamano waliyopanga ili kuzipa nafasi juhudi za kimataifa za kutatua mgogoro wa kisiasa uliotokana na matokeo ya uchaguzi uliofanyika nchini humo Desemba 27.

https://p.dw.com/p/Clc0
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga.Picha: AP Photo

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukutana na mpatanishi wa mgogoro huo, Waziri mdogo wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani Jendayi Frazer, Kiongozi wa Upinzani nchini Kenya Raila Odinga alithibitisha kuanza kwa juhudi za upatanishi, na hivyo kuwaarifu wafuasi wake kwamba maandamano yaliyopangwa kufanyika kesho yamefutwa.

Raila Odinga leo alijikuka katika njia panda, kutokana na shinikizo la kimataifa linalomzuia kufanya jambo lolote ambalo litaweza kuchochea ghasia zaidi, ambapo kwa upande mwingine pia yupo katika msukumo wa kutaka demokrasia ama haki itendeke.

Serikali ya Rais Mwai Kibaki imekuwa ikimlaumu Raila Odinga kwa kuchochea machafuko hayo yanayotokea.

Lakini hata hivyo, Msaidizi wa Odinga, Tony Gachoka alisema hakuna mtu anayetaka kuona umwagaji damu, lakini hakuna njia ya mkato ili kuweza kupatikana kwa demokrasia.

Idadi ya vifo kufuatia vurugu zilizotokea mara baada ya kutagazwa ushindi wa Rais Mwai Kibaki, kufuatia uchaguzi uliofanyika nchini humo Desemba 27, vimeongezeka hadi kufikia 486, na watu wapatao laki mbili na elfu 55 kukosa mahala pa kuishi, tukio ambalo limeelezwa kuwa baya zaidi tangu nchi hiyo ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Waingereza mwaka 1963.

Rais Kibaki tayari amekubali kuunda serikali ya pamoja lakini Bwana Odinga amekuwa akimtaka Rais Kibaki kujiuzulu na kuundwa kwa serikali ya mpito kwa ajili ya kurudiwa tena kwa uchaguzi.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Rais wa Ghana John Kufuor anatarajiwa kutembelea Kenya wiki hiii kujaribu kuleta suluhu kati ya Rais Kibaki na kiongozi wa Upinzani Raila Odinga.

Wakati hali ya utulivu ikiwa inarudi katika maeneo mengi ya nchi hiyo, taarifa zisizothibitishwa kutoka nchini Uganda, zimearifu kuwa Raia wa Kenya wapatao 30, wamezama maji baada ya kukimbizwa na washambuliaji mpakani mwa nchi hizo mbili.

Mkuu wa Wilaya ya Tororo nchini Uganda Mpimbaza Hashaka alisema amepata taarifa kuwa watu 30 wamezamishwa maji katika mto Kipkaren.

Hata hivyo polisi upande wa Kenya bado hawajathibitisha taarifa hizo.

Katika hatua nyingine malori yapatayo 11 ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP yamekuwa yakielekea magharibi mwa Kenya, ambako kumekuwa na wakimbizi wengi, huku yakiwa yamebeba chakula cha kuwatosha watu elfu 38, kitakachotumika kwa wiki mbili.

Ghasia hizo zilizozuka baada ya uchaguzi mkuu nchini humo zimekuwa zikitishia kuporomoka kwa uchumi wa nchi hiyo, ambayo inaongozwa katika eneo la Afrika mashariki.

Wakazi katika mitaa ya mabanda nchini humo na maeneo ya vijijini wanaelezwa kuathirika vibaya na ghasia hizo.