1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiKorea Kusini

Kiongozi wa upinzani Korea Kusini achomwa kisu shingoni

Sylvia Mwehozi
2 Januari 2024

Kiongozi wa upinzani nchini Korea Kusini, Lee Jae-myung, ameshambuliwa kwa kuchomwa kisu shingoni wakati alipokuwa anatembelea eneo la Busan lililotengwa kwa ajili ya kujenga uwanja wa ndege.

https://p.dw.com/p/4anV4
Korea Kusini| Lee Jae Myung
Kiongozi wa upinzani wa Korea Kusini Lee Jae-myung akikimbizwa hospitaliPicha: YONHAP/REUTERS

Kwa mujibu wa taarifa ya vyombo vya habari, Lee Jae-myung alishambuliwa na mtu asiyejulikana na amelazwa hospitali akiwa na fahamu. Polisi imesema Lee ametiwa jeraha la sentimeta moja shingoni.

Afisa mmoja wa chama chake cha kidemokrasia amesema mwanasiasa huyo bado anaendelea kupatiwa matibabu. Chama hicho kimelaani shambulio hilo na kimesema hicho ni kitendo cha ugaidi. Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol, ameagiza kufanyika uchunguzi wa haraka juu ya mkasa huo. Mshambuliaji alikamatwa mara moja kwenye eneo la tukio.

Lee Jae-myung
Kiongozi wa upinzani Lee Jae-myung akizungumza huko BusanPicha: Yonhap via REUTERS

Afisa wa polisi wa Busan Son Je-han amesema mwanasiasa huyo alikuwa amezingirwa na waandishi wa habari wakati mwanamume mmoja alipomchoma upande wa kushoto wa shingo yake.

Katika video zilizorushwa kwenye televisheni za nchini humo, Lee alionekana akianguka chini huku watu wakimkimbilia kumsaidia baada ya shambulio hilo.

Wanasiasa kadhaa mashuhuri wa Korea Kusini wameshambuliwa hadharani katika siku zilizopita.

Lee alishindwa mwaka 2022 na mhafidhina Yoon Suk Yeol katika kinyang'anyiro kikali zaidi cha urais katika historia ya Korea Kusini.