Kiongozi wa Iran awatetea viongozi wa maandamano ya upinzani. | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.08.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kiongozi wa Iran awatetea viongozi wa maandamano ya upinzani.

Kiongozi Mkuu wa Kidini nchini Iran amesema haamini kwamba viongozi wa Maandamano ya upinzani yaliyotokea baada ya uchaguzi wa Rais nchini humo mwezi June walikuwa wakala wa mataifa ya kigeni.

default

Kiongozi Mkuu wa Kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, asema hajathibitishiwa kwamba viongozi wa maandamano ya upinzani walikuwa wakala wa nchi za kigeni.

Akinukuliwa na Televisheni ya taifa ya nchi hiyo, Kiongozi huyo Mkuu wa kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei amesema hawalaumu viongozi hao aliowaita wa matukio ya hivi karibuni kama ni mawakala ya Mataifa ya kigeni ikiwemo Marekani na Uingereza kwa sababu bado haijathibitishwa kwake.

Akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu, amesema hakuna shaka kwamba vuguvugu hilo, kama viongozi wake walilijua ama la, lilipangwa kabla.

Baadhi ya viongozi wenye msimamo mkali wamesisitiza wito wa kukamatwa kwa viongozi wa upinzani waliodai kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu, hali iliyomuwezesha tena Rais Mahmoud Ahmadinejad kuchaguliwa.

Aidha viongozi hao wenye msimamo mkali walidai kwamba Marekani na Uingereza zinahusika na maandamano hayo.

Nalo shirika la Habari la Iran limeripoti kuwa, Rais wa zamani wa nchi hiyo Mohammad Khatami amesema madai yanayowakabili watu hao wenye msimamo wa wastani ya kutuhumiwa kuchochea machafuko baada ya uchaguzi yamefanywa katika mazingira yasiyo ya kawaida na kwamba yalikuwa batili.

Katika kesi iliyosikilizwa siku ya Jumanne, ambayo ni ya nne kusikilizwa tangu kufanyika kwa uchaguzi huo wa mwezi June, Mshirika wa Bwana Khatami Saeed Hajjarian ameripotiwa akisema kuwa amefanya makosa makubwa katika uchaguzi kwa kuwasilisha uchambuzi usio sahihi na kuomba radhi kwa makosa yake hayo.

Mwendesha mashtaka ametaka mtuhumiwa huyo Saeed Hajjarian ambaye anadaiwa kuhatarisha usalama wa taifa, kupewa adhabu ya juu na kwamba kosa hilo linaweza kusababisha adhabu ya kifo.

Wanasiasa wengine waliopandishwa kizimbani kutokana na tuhuma hizo ni pamoja na Naibu Waziri wa zamani wa nchi hiyo pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya nchi za nje, viongozi ambao wote kwa pamoja walitumikia nafasi zao hizo wakati wa uongozi wa Khatami.

Uchaguzi huo wa June 12 umeiingiza nchi hiyo katika mzozo mkubwa wa ndani kisiasa kuwahi kutokea tangu mwaka 1979, wakati wa mapinduzi ya kiislamu.

Mashirika ya Haki za Binadamu yanasema mamia ya watu wakiwemo wanasiasa wanaopenda mabadiliko, waandishi wa habari na wanaharakati waliwekwa kizuizini tangu kufanyika kwa uchaguzi huo, na kwamba wengi wao bado wako magerezani.

Wagombea walioshindwa katika uchaguzi huo wanasema watu 69 waliuawa katika machafuko hayo, lakini serikali inasema ni watu 26 tu.

Wakati hali ya kisiasa ikiendelea hivyo nchini Iran katika upande mwingine wanadiplomasia wa nchi za magharibi wanasema viongozi wa Iran wamelipokea na kulikataa pendekezo linaloitaka nchi hiyo kusimamisha mpango wake wa kurutubisha nyuklia, katika juhudi za kutatua uadui wake wa muda mrefu na nchi za magharibi pamoja na kujiepusha kuwekewa vikwazo vipya na Umoja wa Mataifa.

Wakizungumza bila ya kutaka kutajwa majina, wanadiplomasia kadhaa wamesema pendekezo hilo limetoka kwa wale wenye kukubaliana na ukweli wa mambo ulivyo ndani ya Iran.

Hata hivyo wanadiplomasia hao hawakusema pendekezo hilo lilitolewa na nani, lakini mwanadiplomasia mmoja amesema ni kutoka kwa watu waliokaribu na mwanasiasa wa nchi hiyo aliyeshindwa katika kinyang'anyiro cha kugombea urais, Mohsen Rezai.

Iran imekuwa ikisisitiza kupinga matakwa ya kimataifa ya kuachana na mpango wake huo ambao nchi za magharibi zinawasiwasi kuwa niwa kutengeneza silaha za nyuklia.

Iran inapinga mawazo hayo ya nchi za magharibi kuhusiana na matumizi ya teknolojia hiyo na kusema ni kwa ajili ya matumizi ya kijamii.

Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters)

Mhariri: Abdul-Rahman

 • Tarehe 27.08.2009
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/JJFW
 • Tarehe 27.08.2009
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/JJFW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com