1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimbunga Harvey chasababisha uharibifu

27 Agosti 2017

Kimbunga Harvey kimepiga katikati mwa jimbo la Texas nchini Marekani kikiandamana na mvua kubwa, hali inayoongeza wasiwasi wa kutokea mafuriko ya "majanga” baada ya kusababisha uharibifu katika Ghuba ya Pwani

https://p.dw.com/p/2iuD7
Texas Hurrikan Harvey
Picha: Imago/ZUMA Press/G. Hernandez

Kimbunga Harvey kimepiga katikati mwa jimbo la Texas nchini Marekani kikiandamana na mvua kubwa, hali inayoongeza wasiwasi wa kutokea mafuriko ya "majanga” baada ya kimbunga hicho kikubwa – chenye nguvu Zaidi kuwahi kuikumba Marekani tangu 2005 – kusababisha uharibifu mkubwa katika Ghuba ya Pwani.

Utabiri wa karibuni unaonyesha kuwa kimbunga Harvey, ambacho kimeshushwa hadhi yake na kuwa kimbunga cha Kitropiki, kitazunguka ufukweni katika siku nne au tano zijazo – uwezakano hatari ikizingatiwa kiwango kinachotarajiwa kuongezeka cha mvua.

Texas Hurrikan Harvey
Wakazi wengi wamepoteza makazi yaoPicha: Reuters/A. Latif

Kimbunga hicho, kimeharuibu majumba, kubomoa makazi ya muda, kuyaacha maboti yakiwa yametapakaa mitanaani na kuwaacha mamia kwa maelfu ya watu bila umeme kwenye Ghuba ya Pwani, ambako ni makao ya baadhi ya viwanda muhimu kabisa vya kusafisha mafuta nchini Marekani.

Wakati ni mtu mmoja pekee aliyefahamika kufariki, maafisa wamesema wanahofia kuwa bado kuna maafa yanayotarajiwa, ambapo maeneo makubwa ya Texas yapo chini ya tahadhari za kutokea mafuriko na vimbunga vya hapo na pale vinavyopiga eneo hilo na kuharibu mapaa ya nyumba.

Gavana wa jimbo la Texas Greg Abbott amesema waokozi 1,300 kutoka kikosi cha ulinzi cha taifa wamepelekwa katika maeneo yalioathiriwa na kimbunga, na wanajeshi 500 wa ziada watapelekwa hivi karibuni. Zaidi ya watu 330,000 wameachwa bila ya umeme, na Abbott anasema kutokana na hali ya upepo mkali, itachukua muda kurejesha nishati hiyo

USA Texas Hurrikan Harvey
Wengi wameachwa bila ya umemePicha: Getty Images/AFP/M. Ralston

Rais Donald Trump, ambaye anafahamu uharibifu uliotokea kwa uongozi wa rais wa zamani George W. Bush kutokana na namna alivyozembea katika kushughulikia janga la Kimbunga Katrina, amesema anafuatilia kwa karibu juhudi za msaada akiwa katika makazi ya mapumziko ya Camp David jimboni Maryland.

Kimbunga hicho ni changamoto ya kwanza kuu ya nyumbani kwa Trump, na anapanga kwenda Texas wiki ijayo. Pwani ya Texas ni eneo linalokuwa kwa kasi, ambapo karibu watu milioni 1.5 wamehamia eneo hilo tangu mwaka wa 1999.

Wakazi wengi waliokimbia maeneo yaliyoathirika kabisa jimboni Texas walielekea mji wa San Antonio, ambako makazi ya muda yanasimamiwa na idara ya zimamoto.

Harvey ndicho kimbunga kikali Zaidi kuwahi kulikumba bara tangu Wilma kilipoipiga Floriga miaka 12 iliyopita. 2005 ulikuwa mwaka wa vimbunga – kabla ya Wilma, kimbunga Katrina kiliusambaratisha mji wa New Orleans, na kusababisha vifo vya watu 1,800.

Mwandishi: Bruce Amani AFP
Mhariri: Sudi Mnette