1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kim Jong Ill aendelea kugusa vichwa vya habari Ujerumani

Abdu Said Mtullya29 Desemba 2011

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani hivi leo (29.12.2011) wanazungumzia juu ya Korea ya Kaskazini baada ya kifo cha Kim Jong Ill na pia juu ya Poland kujiunga na Umoja wa sarafu ya Euro.

https://p.dw.com/p/13bIx
Kim Jong Un
Kim Jong UnPicha: AP

Mhariri wa gazeti la Volksstimme anasema enzi mpya zitaanza Korea ya Kaskakazini baada ya kumalizika maombolezo rasmi ya kifo cha Kim Jong Ill. Lakini swali ni iwapo nchi hiyo itaekelekea kwenye njia ya mageuzi au itaendelea na udikteta.

Lakini Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba kutokana na hali mbaya ya uchumi inayosababisha njaa ,Korea ya Kaskakazini haitakuwa na njia nyingine ila kuyaleta mageuzi, hata ikiwa ndani ya mfumo wa kikomunisti.

Gazeti la Neue Osnabrücker pia limeandika juu ya Korea ya Kaskazini, lakini halina matumaini makubwa juu ya kuletwa mageuzi nchini humo. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa dunia nzima imefuatilia kwa makini maombolezo ya kifo cha Kim Jong ill. Mhariri huyo anatilia maanani kwamba kwenye maombolezo hayo palikuwa na ujumbe uliojificha.

Jee kwa nini Kiongozi mpya ,Kim Jong Un alitembea sambamba na gari lililolibeba jeneza, badala ya kutembea mbele ya gari hilo.? Viongozi wa Korea ya Kaskazini jana walionyesha kwamba wanayajali maslahi ya watu wao na siyo kile watu wa nje wanachokitaka! Kwa hivyo anasema mhariri huyo ujumbe ulikuwa wazi kwa wote duniani kwamba, wale wanaojaribu kuikosoa Korea ya Kaskazini hawatapewa nafasi kwa sababu umma wa nchi hiyo umesimama pamoja na serikali.

Mwenyekiti wa Kanda ya Euro, Jean-Claude Juncker
Mwenyekiti wa Kanda ya Euro, Jean-Claude JunckerPicha: picture alliance/dpa

Gazeti la Lausitzer Rundschau linazungumzia juu ya Poland kujiunga na Umoja wa sarafu ya Euro kwa kutilia maanani kwamba habari hizo zimewashtua baadhi ya watu nchini Ujerumani ambao bado wanautumia msemo wa miaka mingi wa kuukebehi uchumi wa Poland. Lakini mhariri wa gazeti la Lausitzer Rundschau anasema kujiunga kwa Poland na Umoja wa sarafu ya Euro ni jambo la baraka! Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba kwa baadhi ya watu nchini Ujerumani,kuingia kwa Poland katika Umoja wa sarafu ya Euro ni kama tishio. Na wanauliza jee udanganyifu uliofanywa na Ugiriki hautoshi, jee kufilisika kwa Italia na Ureno hakutoshi?

Lakini mhariri anesema hiyo ni hukumu inayotolewa kabla ya kufika mahakamani. Anaeleza kuwa litakuwa jambo la baraka ikiwa Poland itajiunga na Umoja wa sarafu ya Euro. Tofuauti na Ugiriki iliyofanya udanganyifu, Poland ni nchi inayojiamini.

Mwandishi Mtullya Abdu/ Deutsche Zeitungen/

Mhariri/ Yusufu, Saumu