1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KIGOMA: Silaha haramu zachomwa

23 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCYZ

Polisi wamezichoma moto bunduki 2,000 haramu hii leo mjini Kigoma Tanzania. Hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa kuwasamehe watu watakaosalimisha silaha zao.

Bunduki hizo zilisalimishwa mwaka jana magharibi mwa Tanzania katika mpango wa kutokomeza silaha haramu nchini humo. Kamishna wa polisi Paul Chagonja amesema uingizwaji wa silaha ndogo ndogo nchini humo umesababisha uchungu na maafa makubwa miongoni mwa watanzania.

Bunduki hizo zimechomwa katika uwanja wa ziwa Tanganyika mjini Kigoma, yapata kilomita 1,000 magharibi mwa Dar es Salaam. Watu takriban 4,000 walioshuhudia tukio hilo walishangilia wakati silaha hizo zilipokuwa zikitetekea.

Tanzania ni mojawapo ya mataifa yaliyosaini mkataba wa Nairobi wa kuzuia, kudhibiti na kupunguza utapakazaji wa silaha ndogo ndogo katika eneo la maziwa makuu na pembe ya Afrika, unaotaka umilikaji wa silaha upigwe marufuku.