1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KHARTOUM:Rasimu ya azimio la Darfur kuidhinishwa

31 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBdV

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linasogea karibu na hatua ya kuidhinisha rasimu ya azimio litakalofanikisha hatua ya kupeleka kikosi kilichoimarishwa cha majeshi ya Umoja wa Mataifa na Afrika kwenye eneo la Darfur nchini Sudan.Uingereza na Ufaransa wanaofadhili rasimu hiyo wametoa nakala mpya ya azimio lililopunguzwa makali linalosubiri kupigiwa kura.

Kwa mujibu wa naibu balozi wa Ufaransa Jean-Pierre Lacroix rasimu hiyo mpya huenda ikawa tayari kupigiwa kura hii leo.

Nakala mpya ya rasimu hiyo inaeleza kuwa kikosi hicho maalum kitajulikana kama UNAMID na kuanza kutekeleza shughuli zake ifikapo mwezi Disemba mwaka huu na kuchukua majukumu ya kikosi cha Umoja wa Afrika cha AMIS kilichoko Darfur kwa sasa.

Wiki jana rasimu ya azimio hilo ilipunguza makali ambayo yangehatarisha makubaliano ya amani ya Darfur yaliyofikiwa mwaka jana kati ya Serikali ya Sudan na kundi kuu la waasi vilevile kuwekea nchi hiyo vikwazo zaidi.Azimio hilo jipya linakipa kikosi kipya uwezo wa kutumia nguvu ili kujilinda na kuwalinda raia wanapolinda amani.