1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KHARTOUM : Wanadiplomasia wa magharibi watimuliwa

24 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBWY

Sudan imewatimuwa mwanadiplomasia mwandamizi wa Canada na mjumbe wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya kutoka nchini humo kwa kile ilichokielezea kuwa kuingilia kati masuala ya ndani ya nchi.

Shirika la habari la taifa limesema wanadiplomasia hao wawili waliitwa kwa nyakati tafauti wizara ya mambo ya nje na kukabidhiwa hati za kutimuliwa kwao nchini humo.Bado haiko dhahiri hasa kwa nini wanadiplomasia hao wanatimuliwa lakini nchi nyingi za magharibi zimekuwa zikishutumu serikali ya Sudan kwa dhima yake katika mauaji yanayofanyika kwenye jimbo lenye vurugu la Dafur ambapo watu laki mbili wameuwawa na wengine milioni mbili wamepotezewa makaazi yao tokea kuzuka kwa mzozo wa jimbo hilo miaka minne iliopita.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje amesema harakati za wanadiplomasia hao zinamaanisha kuingilia kati masuala ya ndani ya nchi ya Sudan na hiyo kwenda kinyume na majukumu yao ya kibalozi.

Ali Al Sadeq hata hivyo amesema Sudan inataka sana kudumisha uhusiano wake na Halmashauri ya Umoja wa Ulaya na Canada.