KHARTOUM: Sudan yapongezwa kwa kukubali kikosi Darfur. | Habari za Ulimwengu | DW | 14.06.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

KHARTOUM: Sudan yapongezwa kwa kukubali kikosi Darfur.

China, ambayo ni mshirika mkuu wa Sudan, imeipongeza serikali hiyo kwa kukubali kikosi mchanganyiko cha majeshi ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kipelekwe katika eneo la Darfur linalokabiliwa na mzozo.

Afisa wa kibalozi wa Sudan jana alithibitisha mjini Addis Ababa, Ethiopia kwamba serikali yake imekubali wanajeshi kati ya alfu 17 na alfu 19 wa Umoja wa Afrika pamoja na Umoja wa Mataifa wapelekwe katika eneo hilo.

Sudan iliuchukua uamuzi huo baada ya kuhakikishiwa kwamba kikosi hicho kitakuwa na mamlaka maalum kwenye eneo husika huku serikali hiyo ikibaki kulinda mipaka yake.

Wakati huo huo Afisa Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia shughuli za amani za Umoja huo, John-Marie Guehenno ameisifu Sudan kwa uamuzi huo iliochukua.

John-Marie Guehenno amesema:

"Tutajitahidi kwa vyovyote vile kuhakikisha kikosi hicho msingi wake utakuwa bara la Afrika. Hivyo ndivyo tulivyokubaliana. Tunaamini hilo litawezekana kwa sababu tayari mataifa kadha ya Afrika yamejitolea kuleta wanajeshi. Hata hivyo kuna majukumu fulani ambayo itatubidi tuzingatie mahali kwengine. Nimefurahi sana hasa kwa kuwa wakati wa mashauriano yetu, ujumbe wa Sudan ulilikubali hilo"

John-Marie Guehenno alikuwa akihutubia waandishi wa habari mara baada ya kushauriana na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com