1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Charles Taylor yaanza tena.

7 Januari 2008

Kesi ya dikteta wa zamani wa Liberia Charles Taylor imeanza tena mjini The Hague nchini Uholanzi baada ya kuahirishwa mwezi Juni mwaka jana.

https://p.dw.com/p/ClVf
Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor alipofikishwa mara ya kwanza katika mahakama ya uhalifu wa kivita Mjini FreeTown Aprili 3, 2006.Picha: AP

Kesi inayofanyika mjini The Hague katika mahakama maalum ya uhalifu wa kivita dhidi ya dikteta Charles Taylor wa Liberia inaingia katika hatua ya uamuzi. Dikteta huyo mwenye umri wa miaka 59 anapaswa kujibu mashtaka kuhusu uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone.

Kama shahidi wa kwanza , mwendesha mashtaka mkuu hii leo ameanza na mtaalamu anayehusika na biashara ya Almasi zinazoitwa zenye damu katika Afrika magharibi kuweza kutoa taarifa yake pamoja na mchimba migodi ya Almasi ambaye amekatwa mikono. Kwa jumla mwendesha mashtaka Steven Rapp atawaleta mashahidi 144, ikiwa ni pamoja na wahanga karibu 80 wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kutoka Sierra Leone pamoja na wengine wengi wafanyakazi wa karibu wa dikteta huyo wa zamani Charles Taylor. Charles Taylor anashitakiwa kwa makosa karibu kumi na moja , ya kuuwa, ubakaji wa wanawake na watoto, utesaji , kuwatumia watoto kama wanajeshi, na kuwatumia watu kama watumwa, kwa kuwafanyisha kazi ngumu katika uchimbaji wa Almasi.

Mshitakiwa hakuchafua mikono yake tu kwa makosa hayo, lakini mwendesha mashtaka amesema pia kuwa , Taylor akiwa rais wa Liberia ameunga mkono uasi wa kundi la United Revolutionary Front katika nchi jirani ya Sierra Leone, kwa fedha, silaha pamoja na wanajeshi wauaji ambao wamepata mafunzo maalum. Kiongozi wa kikosi hicho pamoja na Taylor walikuwa marafiki.

Wakati huo huo familia na marafiki wa Charles Taylor walifanya maombi maalum kanisani jana Jumapili wakimuunga mkono rais huyo wa zamani wa Liberia, kabla ya kesi yake hii leo. Kwa upande wake kwa kusaidia kwake rais huyo wa zamani wa Liberia katika biashara hiyo ya Almasi alifaidika na biashara hiyo.

Waasi hao walifanya mauaji ya kinyama. Wamewakata viungo watu wasio na hatia pamoja na kuwakata midomo na masikio. Kati ya mwaka 1996 na 2002, amesema mwendeshaji mashaka kuwa watu zaidi ya 20,000 wamekuwa wahanga wa wapiganaji hao wa chini kwa chini. Na kati ya mwaka 1989 na 2003 inakadiriwa kuwa mzozo huo umesababisha watu 400,000 kuuwawa, ikiwa ni pamoja na 120,000 nchini Sierra Leone.

Kutokana na msingi wa usalama kesi hii

dhidi ya kiongozi huyo wa zamani wa Liberia ilihamishwa kutoka Sierra Leone na kupelekwa katika mji mkuu wa Uholanzi The Hague. Kwa ajili ya kesi hii hata hivyo mahakama hii changa ya kimataifa inajaribu kutoa uamuzi wake. Baada ya ufunguzi uliozingirwa na mtafaruku mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka jana , kutokana na wakili wa Taylor kutoka katika chumba cha mahakama na kusababisha kesi hiyo kuahirishwa. Courtenay Griffiths, raia wa Uingereza sasa atakuwa wakili wa mshtakiwa, ambaye amekwishafanyakazi kwa muda wa nusu mwaka sasa katika wadhifa huo. Taylor anakana mashtaka yote na aitambui mahakama hiyo ya Sierra Leone.

Mahakama hii haisimamiwi na umoja wa mataifa , lakini inapata usaidizi wa kifedha kutoka mataifa wanachama wa umoja wa mataifa. Katika bajeti kwa ajili ya mahitaji maalum, mshtakiwa kila mwezi hupatiwa fedha maalum.Mwendesha mashtaka lakini huchunguza kila wakati matumizi ya Charles Taylor kutoka na fedha hizo.