Kenya yafikiria sera ya mwanamke 1 watoto 2
6 Novemba 2013Ripoti ya utafiti huo iliyopewa jina la "Uchambuzi wa Hali ya Idadi ya Watu nchini Kenya" na kuchapishwa rasmi mwishoni mwa mwezi uliopita na Wizara ya Mipango ya nchi hiyo, inasema haja ya watoto ni kubwa sana nchini humo na kwamba lazima idhibitiwe.
Maeneo kame ya kaskazini mwa nchi hiyo, licha ya kuwa kwake na shida kubwa zaidi ya maisha, yametajwa na ripoti hiyo kuwa yanayoongoza kwa idadi kubwa ya vizazi.
Ingawa ripoti hiyo haisemi moja kwa moja, lakini inaelekea sana kupendekeza sera ya kila mwanamke kuzaa watoto wawili nchini Kenya kuwa jambo la lazima.
Kazi kubwa zaidi yahitajika
Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema kwamba hata kama sera hiyo itaanzishwa, italazimika kutanguliwa na mfumo mzuri sana wa kuisaidia, zikiwemo njia za kuimarisha uzazi salama, afya ya kimama na watoto wanaozaliwa na pia kampeni itakayokwenda hadi vijijini.
Kubwa zaidi ni kuhakikisha kuwa wasichana wengi zaidi kadiri inavyoyumkinika wanapatiwa elimu angalau mpaka ya sekondari, kwani utafiti huo ulionesha kwamba wanawake wenye watoto kidogo zaidi ni wale ambao angalau wamefikia kiwango hicho cha elimu.
Wakosoaji wa pendekezo hili la kuanzishwa kwa sera ya watoto wawili kwa kila mwanamke, wanasema kwamba hakuna uwiano kati ya idadi ndogo ya watu na kufikiwa kwa Dira 2030 inayoielekeza Kenya kuwa taifa lenye uchumi wa kati.
Mwandishi: Mohammed Khelef/standardmedia.co.ke
Mhariri: Josephat Charo