1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yaadhimisha miaka 54 ya Uhuru

12 Desemba 2017

Kenya hii leo inaadhimisha miaka 54 ya kujitawala yenyewe baada ya kujipatia Uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka 1964.

https://p.dw.com/p/2pCAB
Kenia Unabhängigkeitstag 12.12. 2013
Picha: Reuters

Sherehe za kuadhimisha siku hiyo zinafanyika katika uwanja wa Kimataifa wa Moi, Kasarani jijini Nairobi ambako wakenya wanasubiri kwa hamu hotuba ya rais Kenyatta inayotarajiwa kugusia Umoja wa Kitaifa.  Hii itakuwa hotuba ya kwanza ya rais Kenyatta tangu alipoapishwa tarehe 28 Novemba kama rais wa kenya baada ya kukamilika kipindi kigumu cha  uchaguzi.

Wakenya walianza kumiminika katika uwanja wa Moi Kasarani mapema  leo asubuhi huku usalama ukiimarishwa na kila aliyekuwa akiingia uwanjani humo kuanzia saa moja asubuhi akipekuliwa kabla ya kuruhusiwa ndani. Katika sherehe hizo, aliyekuwa wa Ghana John Mahama amehudhuria  huku viongozi wa upinzani wakisemekana kuzisusia.

Kenia Jamhuri-Feier
Wakenya katika uwanja wa Moi wakiadhimisha siku ya JamhuriPicha: DW/Shisiya Wasilwa

Gwaride la kijeshi ndilo lililofungua rasmi maadhimisho haya ya siku ya Jamhuri, na baadaye jeshi la angani likaonyesha ustadi wake kwa kupaaa angani huku likitoa moshi unaofanana na bendera ya Kenya. Wakenya wanaohudhuria sherehe hizo pia wameburudishwa na ngoma na nyimbo  mbali mbali, waimbaji wa kizazi kipya na hata nyimbo za kitamaduni.

Hata hivyo kilele za sherehe hiyo ni hotuba ya rais Kenyatta inayosubiriwa kwa hamu inayotarajiwa kugusia masuala ya kipindi kirefu cha uchaguzi kilichomalizika hivi karibuni, elimu ya bure ya shule za sekondari, Umoja wa wakenya wote, usalama na miundo mbinu.

Hii itakuwa ni siku yake ya kwanza ya Kitaifa kwa Rais Kenyatta baada ya kuapishwa mwezi Novemba katika awamu yake ya pili na ya mwisho kama rais wa Kenya. Hii ni baada ya Mahakama ya juu kutupilia mbali kesi iliyowasilishwa kupinga ushindi wa Rais Kenyatta katika uchaguzi mpya uliyofanyika tarehe 26 Oktoba.

Kenia Wahlwiederholung Raila Odinga
Kiongozi wa Upinzani Raila OdingaPicha: picture-alliance/dpa/D. Bandic

Upinzani wasusia sherehe za Jamhuri

Aidha siku ya Jumapili viongozi wa muungano wa upinzani NASA waliahirisha sherehe ya kumuapisha kinara wao Raila Odinga kama rais mbadala wa Kenya na Kalonzo Musyoka kama makamu wake.

NASA imeahirisha shughuli hiyo kutokana na shinikizo kutoka kwa wanadiplomasia wa kigeni na viongozi wa kidini.

Mjini Mombasa inayojulikana kama ngome ya upinzani, hapakuwa na shamra shamra ya siku hii ya Jamhuri, idadi ndogo ya watu ilishuhudiwa katika uwanja wa Tononoka ambapo sherehe hiyo itafanikishwa na machifu wa eneo hilo.

Hali ya usalama imeimarishwa. Kwengineko mjini Taita Taveta wakaazi wanasherehekea siku hiyo katika uwanja wa Voi. Sherehe nyengine zinafanyika katika kaunti mbali mbali ya taifa hilo la Afrika Mashariki.

Mwandishi: Amina  Abubakar- Nation Media

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman