1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya kuwanunulia wawakili wa kaunti magari ya dola mil.41

Shisia Wassilwa10 Februari 2021

Tume ya Kusimamia Mishahara ya wafanyakazi wa Umma nchini Kenya-SRC, imeidhinisha ruzuku ya magari ya shilingi bilioni 4.5 sawa na dola milioni 41 za Marekani kwa waakilishi wote wa Kaunti nchini humo.

https://p.dw.com/p/3pAZB
Uhuru Kenyatta  Kenia
Picha: Getty Images/T.Karumba

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, mwenyekiti wa SRC Lyn Mengich amesema hatua hiyo inalenga kusawazisha usawa na haki kwa wabunge.

Aidha barua hiyo imeongeza kusema kuwa, waakilishi wote wa kaunti na maspika waliokuwa wamechukua mikopo ya kununua magari sasa hawatahitajika kulipa.

Tamko lake linajiri majuma mawili baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuwaahidi waakilishi hao ruzuku ya magari. Waakilishi hao walitoa shuruti la ruzuku hiyo kabla ya kuupitisha mswada wa mpango wa maridhiano wa BBI.

Soma pia: Madaktari wa Nairobi waanza mgomo

Tayari kaunti ya Siaya na Kisumu zimepitisha mswada huo, ulioungwa mkono na Raila Odinga, ambaye ni mshirika wa rais Kenyatta kwenye masuala ya BBI.

Huku naibu Rais William Ruto na washirika wake wa siasa wakisema kuwa ruzuku ya magari kwa wawakilishi wa kaunti ni sawa na hongo, hatua hiyo sasa huenda ikabadilisha mwelekeo wake.

Hatua hiyo inajiri wakati deni la taifa la Kenya linapozidi kuongezeka huku Benki ya Dunia na Shrika la Fedha Ulimwenguni, vikiionya serikali kuhusu matumizi mabaya ya fedha.

Kenia Ärzte Protest
Madaktari nchini Kenya wakiandamana katika mojawapo ya migomo ya kudai kuboreshewa maslahi yao, ambapo serikali imekuwa ikisistiza kuwa haina fedha.Picha: Reuters/T. Mukoya

Madaktari na Wauguzi wamekuwa wakigoma, wakitaka nyongeza ya mishahara na kuboreshwa kwa mazingira ya utendaji kazi wao kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Wananchi wamelaani hatua hii ya serikali, ambayo imekuwa ikiwatisha kuwafuta watumishi wa afya wanaogoma wakitaka kuboresha maslahi yao, ikisema haina fedha.

Takriban kaunti 24 kati ya 47 zinahitaji kuupitisha mswada wa BBI kabla ya kuwasilishwa bungeni na hatimaye kufanyika kwa kura ya maoni ambayo itabadilisha katiba.

Soma pia: Miezi mitatu ya mgomo wa wauguzi Kenya

Taifa la Kenya lina waakilishi 2224 wa kaunti, iwapo kila mmoja wao atapokea shilingi milioni mbili sawa na dola elfu 18, mkenya anayelipa kodi atabebeshwa mzigo wa shilingi bilioni 4.5 sawa na dola milioni 41.

Waakilishi wa kaunti wanaonekana kuwa watu muhimu kwenye mchakato wa kuupitisha mswada wa BBI, licha ya kuwa utafiti unaonesha kuwa Wakenya wengi hawana imani nayo, kwani inalenga kubuni nafasi zaidi kwa viongozi.