1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kauli ya Mkurugenzi mkuu wa DW Erik Bettermann

Abdu Said Mtullya2 Mei 2013

Tarehe kama ya leo miaka 60 iliyopita, DW ilianza kutangaza. Jee leo DW imesimama wapi baada ya muda huo. Ni mambo gani yaliyobadilika kimsingi. Maswali hayo yanajibiwa na Mkurugenzi Mkuu wa DW Erik Bettermann.

https://p.dw.com/p/18ItW
Intendant der Deutschen Welle
Erik BettermannPicha: DW

Nini hasa kimejitokeza kwa nguvu katika wadhifa wako wa miaka 12, na tokea kuanza kwa karne mpya?

Bettermann:  Kisiasa, bila shaka ni mashambulio ya tarehe 11 Septemba 2011 na athari zake kubwa. Siku chache baada ya kuingia katika wadhifa huu, niliweza kuthibitisha umuhimu wa DW kwa nchi yetu, umuhimu wa kutumia sauti yetu wenyewe kutambulika. Mbali na hayo ni maendeleo ya haraka ya tekinolojia. Maendeleo hayo yamelata mapinduzi katika tasnia ya mawasiliano duniani. Hayo yanahusu uzalishaji na uenezi wa vyombo vya habari, sambamba  na njia za kutumia mitandao: hayo yamebadilika sana.

Miaka minane baada ya kumalizika vita kuu vya pili, DW ilipewa jukumu la kuishindikiza Ujerumani katika njia ya kurejea katika jumuiya ya kimataifa. Jee DW leo ina majukumu gani baada ya kuanza kutangaza miaka 60 iliyopita?

Bettermann: Kama ilivyokuwa wakati huo, leo pia jukumu la DW ni kuitangaza nchi yetu na maadili yake. DW inapaswa kuifanya Ujerumani ieleweke kama nchi iliyokomaa katika utamaduni wa kiulaya na pia kama nchi huru ya kidemokrasia inayoongozwa katika misingi ya kisheria kama inavyofafanuliwa katika sheria ya mwaka wa 2005. Sheria hiyo imeleta usasa na kulipanuza lengo la matangazo yetu. Kutokana na lugha mbalimbali zinazotumika na kutokana na kitengo cha taaluma, tumeweza kutoa jukwaa la mdahalo wa kitamaduni na majukwaa ya aina nyingine. Ndiyo sababu kwamba tunatambua kuwa sauti ya uhuru na ya haki za  binadamu. Pamoja na hayo tunaiendeleza lugha ya Kijerumani. Hilo pia ni sehemu ya jukumu letu.

Na jee vipi kuhusu majukumu  ya kiandishi?

Bettermann: Tunataka kuifikia hadhira yote duniani. Na kwa ajili hiyo tunayatayarisha maudhui katika lugha 30, kiandishi. Jukumu la kisheria na mwongozo wa DW unatoa muundo kwa idara zetu. Mwongozo wa kazi yetu, wakati wote pia ni matarajio ya watazamaji, wasikilizaji na watumizi wa mtandao wetu. Tunapaswa kuwasiliana nao katika sehemu mbalimbali za dunia katika  lugha mbalimbali kwa kadri  itakavyowezekana. Kutokana na maendeleo ya kitekinolojia na kutokana na kuendelea kubadilika kwa matumizi ya mtandao huu ni mchakato wa kuenda sambamba na maendeleo. Hii ndiyo sababu kwamba, tokea miaka mingi tunatumia masafa mafupi, tumepanuza televisheni ya satelaiti na tulianza mapema matumizi  ya  mtandao wa internet na leo tunafanyakazi kwa kuzichanganya tanzu hizo zote za vyombo vya habari. Na ndiyo sababu tunayaelekezaa madhui yetu kikanda kwa kadri inavyowezekana. Sasa ni mwaka mmoja tokea tuanze kueneza habari kwa kupitia katika mikondo sita ya televisheni za kanda, katika lugha za kijerumai, kiingereza, kiarabu na kihispania. Pia tunatayarisha vipindi vya televisheni kwa vituo tunavyoshirikiana navyo barani Asia, Kusini mashariki mwa Ulaya na Brazil. Na kuhusu shughuli za  mtandao na mitandao ya kijamii ni sehemu ya huduma tunazotoa.

Mnapewa majukumu kisheria, mnalipiwa na serikali-licha ya hayo mmeendelea kuwa huru kiandishi, hata baada ya miaka 60. Vipi imewezekana kwa DW katika mazingira hayo kujijenga kamasauti ya kuaminika?

Bettermann: Kama kituo cha umma cha matangazo ya nje kinacholipiwa kwa fedha za walipa kodi tunayo nafuu muhimu kwenye ulingo wa habari  wa kimataifa: kama ilivyo kwa radio za ndani sisi pia tunao uhuru na tunalindwa kwa mujibu wa ibara ya  tano ya katiba ya nchi. Ndiyo sababu hakuna mikingamo baina ya majukumu yetu kisheria, na kulipiwa kwetu na wala hakuna mikingamo na uhuru wa kazi zetu za kiandishi.Kutokana na uandishi mzuri, na kutokana na kuiwasilisha nchi yetu kwa uzito sawa, katika miaka mingi, DW imeweza kujipambanua kwa sifa ya kuwa chanzo cha habari cha kuaminika. Sera yetu ya kuwapa sauti wale wanaokandamizwa katika  nchi zao,imechangia katika sifa hiyo.Tulifanya hivyo mnamo miaka ya 70 wakati wa udikteta nchini Ugiriki, leo pia kwa mfano tunafanya hivyo kuwapa sauti wasomi wanaozikosoa serikali zao au wasanii nchini China na wanaharakati wa Iran na katika nchi za kiarabu. Watu wanatuamini. Hiyo ni hazina kuu kwa kituo cha  kimataifa kinachotangaza duniani kote.

Jee hiyo ndiyo sababu kwamba  mafunzo yanayotolewa na kitengo cha taaluma cha DW yana utashi  mkubwa?

Betterman: Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita tumekuwa tunaendeleza mifumo huru na ya uwazi ya vyombo vya  habari duniani kote.Na katika hilo mshirika wetu muhimu kabisa ni wizara ya  Ujerumani ya ushirikiano  wa kiuchumi na maendeleo. Kwa pamoja tunaimarisha ubora  wa  wa uandishi na uwezo wa vyombo vya habari katika nchi zinazoendelea na katika nchi zinazojikwamua kimapinduzi. Kwa mfano tumo katika harakati nchini Tunisia na Syria, tunasaidia katika juhudi za kuleta uwazi nchini Myanmar na tunashiriki katika miradi ya muda mrefu katika nchi za Amerika ya kati, Miradi tunayoiunga mkono, inavuka shabaha za kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari. Tunachofanya pia ni kueneza mikakati ya taasisi za vyombo vya habari juu ya kujikwamua kiuchumi na kuwapa watu wanaopunjika fursa ya kupata habari. Mara nyingi tumevisaidia vituo vya radio vya serikali kuelekea katika muundo wa kisheria wa kwa manufaa ya umma. Mfano ni kazi tunayoifanya sasa katika Jamhuri ya Moldova. Utashi ni mkubwa kiasi kwamba hatuwezi kuyatimiza mahitaji ya wote. Kwa sasa watu, 3000 kutoka vyombo vya habari, kila mwaka wanashiriki katika mafunzo ya juu. Tunaweka mkazo katika kutoa mafunzo hayo katika nchi husika katika msingi wa muda mrefu. Ruwaza  yetu ya masomo ya vyombo vya habari ya kimataifa inawapa washirika wetu uwezekano wa ziada wa kujipatia ustadi. Kitengo cha mafunzo cha DW ndiyo taasisi ya Ujerumani inayoongoza katika maendeleo ya vyombo vya habari vya kimataifa.

DW imepiga hatua kutoka kwenye matangazo ya masafa mafupi na kuwa taasisi ya mtangamano wa njia zote za vyombo vya habari. Jee hatua hiyo imetokana na ulazima wa kujibadilisha?

Bettermann: Tokea mwaka 1953 pametokea mabadiliko makubwa sana katika mazingira ya utangazaji wa radio na njia za mawasiliano duniani. Kituo chochote ambacho hakijaribu kuenda sambamba na changamoto hizo, na kuwa na wepesi wa kufanya mabadiliko wakati wote, hakika kitaachwa nyuma haraka. Tuliwahi mapema kuanzisha mfumo wa "digital". Tukiwa ni Radio ya serikali, tulikuwa wa kwanza nchini Ujerumani kuingia katika mfumo wa internet. Tulikuwa mbele kabisa katika kuleta mabadiliko na kuingia katika mfumo wa mtangamano wa njia zote za habari. Yeyote  anaefanya mafunzo kwetu atapata ustadi wa tanzu zote za habari: matumizi ya Kamera, Mikrofoni (vipaza sauti) na mtandao wa internet. Mitandao ya kijamii katika  lugha zote 30, siku nyingi imekuwa kazi zetu za kiandishi za kila siku. Lakini katika kuleta usasa pia tunajikusuru mambo fulani. Ndiyo sababu tumeyafunga baadhi ya matangazo kwa kuwa hayana tena wasikilizaji. Masharti ya kupata fedha    zilizohitajika kwa ajili ya kuendeleza televisheni na mtandao wa Internet, yalikuwa kuyafunga matangazo ya masafa mafupi. Hata hivyo uwezo wa kuyaendeleza mabadiliko haya kwa nguvu zetu wenyewe, bila ya msaada zaidi, umetumika kwa ukamilifu. Tokea mwishoni mwa miaka ya 1990,  DW imepungukiwa zaidi ya theluthi moja ya bajeti yake.

Kwa maoni yako ni zawadi gani  muhimu sana, ambayo DW ingependelea kutunukiwa katika kuadhimisha miaka 60 ya uwepo wake?

Bettermann: Tokea siku ya kwanza kabisa, DW imelitimiza kwa moyo wote jukumu   muhimu katika uhusiano wa nchi yetu na nchi nyingine. DW inahakikisha kusikika kwa sauti na maoni ya vyombo vya habari vya Ujerumani miongoni mwa jumuiya ya  kimataifa. Jukumu hilo limezidi kuwa muhimu zaidi katika mwongo uliopita. Nchi nyingi zimepitisha juhudi kubwa katika kuanzisha harakati za vyombo vya habari kuvuka mipaka yao na kuziimarisha. Nchi hizo zimeutambua umuhimu  wa mawasiliano ya kimataifa katika kuyaeneza malengo yao ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni. Ushindani wa kuzigusa nyoyo za watu duniani umezidi kuwa mkali. Ninachopendelea kukiona hapa nchini ni mwafaka wa kisiasa na kijamii utakaohakikisha kwamba Ujerumani hairudi nyuma. Tunapaswa kuyatumia zaidi mawezekano yanayotokana na mfumo wa vyombo vya habari katika kuieneza nchi yetu katika nchi za nje. Uanuai wa vyombo vya habari na ubora mkubwa uliopo nchini, ambao tunauthamini sana, unapaswa kutumiwa ili kuwafikia, wasikilizaji, wasomaji na watazamaji wa New York, Singapur, Kairo na Buenos  Aires. Lazima tuipe hadhira kilicho bora kabisa kutoka Ujerumani. Ndiyo sababu natumia nguvu zangu zote ili kituo chetu cha mawasiliano na nje, kitangamanishwe na mfumo wa ndani wa vyombo vya habari. Itakuwa zawadi adhimu kabisa ikiwa mazungumzo husika   yatamalizika kwa mafanikio katika maadhimisho ya mwaka wa 60 wa DW.

Tafsiri:Mtullya Abdu.
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman