Kashfa ya kunasa mawasiliano ya simu yamuathiri Cameron | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.07.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kashfa ya kunasa mawasiliano ya simu yamuathiri Cameron

Waziri mkuu David Cameron huenda akasalimika katika kashfa ya kunasa mazungumzo ya simu katika himaya ya vyombo vya habari ya Rupert Murdoch, lakini hadhi yake imeathirika.

default

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron, hadhi yake imeathirika kutokana na akshfa hii.

Waziri mkuu David Cameron huenda akasalimika katika kashfa ya kunasa mazungumzo ya simu katika himaya ya vyombo vya habari ya Rupert Murdoch, lakini hadhi yake imeathirika na tayari hali isiyothabiti ya uaminifu kwa umma katika siasa za Uingereza, biashara na vyombo vya habari imedhoofika zaidi.

Kashfa kuhusiana na madai kuwa waandishi habari katika gazeti linalomilikiwa na tajiri mkubwa Rupert Murdoch la News of the World , walisikiliza kinyume na sheria mazungumzo ya simu za wahanga wa mauaji na familia za wanajeshi waliouwawa katika vita imepelekea kufungwa kwa gazeti hilo na kujiuzulu kwa baadhi ya wasaidizi wa juu wa Murdoch, pamoja na mkuu wa polisi nchini Uingereza.

Maamuzi ya Cameron yametiliwa shaka baada ya kumuajiri mhariri wa gazeti hilo , Andy Coulson , kuwa mkuu wa kitengo cha habari katika ofisi ya waziri mkuu, na uhusiano wake na Rebekah Brooks , ambaye amejiuzulu kuwa mtendaji mkuu wa tawi la magazeti ya Murdoch nchini Uingereza, sasa unaonekana kuwa wa kufurahisha. Baada ya afisa wa pili mwandamizi wa polisi kujiuzulu jana na hatua mpya katika za maendeleo ya habari hiyo kila wakati zikizuka, utabiri wa wapi taarifa hii inaweza kuelekea hauwezekani. Iwapo Cameron hatakuwa na bahati , wadadisi wanasema , inaweza kuelezea kipindi chake cha uwaziri mkuu.

Großbritannien Abhörskandal Boulevardzeitung News of the World Andy Coulson verhaftet

Mhariri wa zamani wa News of the World Andy Coulson

Cameron mwenye umri wa miaka 44, amefupisha ziara yake katika bara la Afrika ili kushughulikia mzozo huo na amesema kuwa bunge litachelewesha mapumziko yake ya majira ya joto kumuwezesha kuwahutubia wabunge kuhusiana na kashfa hiyo.

Kutakuwa na mbinyo wa aina fulani dhidi ya Cameron lakini hii inakwenda mbali zaidi ya yeye binafsi, amesema David Lea , mchambuzi wa masuala ya Ulaya magharibi katika kitengo cha ushauri cha udhibiti wa hali tete kilicho na makao yake mjini London.

Hii inajumuisha hali katika uongozi mzima , ambapo madai mabaya zaidi huenda ni yale yanayowahusisha polisi, hayawezi kuiangusha serikali lakini hayatasahaulika pia.

Lea amesema kuwa Cameron atapata shida kuepuka kashfa hii bila kuchafuka, kama vile Tony Blair katika miaka ya mwisho ya utawala wake alipoandamwa na kuhusika kwa Uingereza katika vita vya Iraq na masuala juu ya kile vyombo vya habari vilivyoita , waraka uliofanyiwa hila , ambao umesaidia kutengeneza uhalali wa kwenda vitani.

Blair alishinda uchaguzi baada ya vita vya Iraq, lakini umaarufu wake haukuweza kutengenezeka tena na hadhi yake iliyoharibika hatimaye ilichangia kuondolewa kwake katika mapinduzi ya ndani ya chama chake. Chama chake cha Labour sasa ni chama cha upinzani. Lakini wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanatarajia kwamba nafasi ya Cameron katika kupigiwa kura haitaporomoka sana , kimsingi kwasababu , kama ilivyo katika kashfa ya madai ya matumizi ya bunge miaka miwili iliyopita , vyama vyote vikuu viwili vimeathirika sana na kashfa hiyo.

Großbritannien Tony Blair verläßt Downing Street

Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza ,Tony Blair aliathirika na mpango wa kuipeleka nchi hiyo vitani.

Si kitu kikubwa ambacho tunafikiri kitakuwa na athari kuhusu nia ya wapiga kura, hususan kwasababu hatimaye inahusu vyama vyote vikubwa, amesema Helen Cleary , mkuu wa utafiti wa kisiasa kwa ajili ya shirika la uchunguzi wa maoni ya wapiga kura la Ipsos Mori. Labour bado kiko mbele katika uchunguzi wa maoni ya wapiga kura, lakini suala kuu bado ni uchumi.

Uongozi wa kisiasa nchini Uingereza umekuwa kwa muda mrefu watumwa wa wamiliki wa vyombo vya habari , hususan Murdoch na magazeti yake yanayomilikiwa na kampuni lake la News International nchini Uingereza.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre

Mhariri : Mohammed Abdul Rahman

 • Tarehe 19.07.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/11ze4
 • Tarehe 19.07.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/11ze4

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com