Kansela wa Ujerumani., Angela Merkel, ziarani katika Mashariki ya Kati kama dalali wa amani. | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.02.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kansela wa Ujerumani., Angela Merkel, ziarani katika Mashariki ya Kati kama dalali wa amani.

Juhudi za kutafuta amani katika eneo la Mashariki ya Kati zinakumbana na mitihani ya kila siku kama vile yanavokumbana maeneo makubwa ya sehemu hiyo na shida za majangwani na hatari za ukame na dhoruba za michanga.

Sheikh Khalifa bin Zayed al-Nahyan, (kulia),akizungumza na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.

Sheikh Khalifa bin Zayed al-Nahyan, (kulia),akizungumza na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu.

Uhakika wa kisiasa unakosekana, kama vile asivokuwa na uhakika mtu anaetembea jangwani kwamba atawasili katika kidimbwi cha maji kilioko mbele yake. Lakini, angalau kidogo, sasa msafara wa kutafuta amani umeanza kupigwa jeki baada ya kuwa katika hatari ya kuvunjika kabisa mnamo miaka michache ya karibuni. Usoni katika kulipiga debe jambo hilo ni Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambaye hivi sasa anashikilia urais wa Umoja wa Ulaya na waziri wake wa mambo ya kigeni, Frank-Walter Steinmeier. Wote sasa wanazungumzia kwamba angalau kuna dirisha lililofunguka kidogo la uwezekano wa kupatikana mwanya kuelekea njia ya amani. Lakini, wakati huo huo, kuna watu wanaosema kwamba kibarua hicho wanachokifanya wanasiasa hao wa Kijerumani hakitafua dafu kutokana na utata wa madaraka ulioko huko Palastina na pia Israel.

Akizungumza wiki hii katika mji mkuu wa Misri, Kairo, baada ya kufanya mazungumzo na Rais Husni Mubarak, akiwa njiani katika safari ya nchi nne-Misri, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Kuwait, Kansela Angela Merkel alisema:

+Nimezungumzia uwezekano wa utaratibu wa amani pamoja na Rais wa Misri. Nimelitaja suala hilo kwa sababu utulivu na amani ni masharti pia ya kupatikana maendeleo imara ya kiuchumi.+

Bila ya shaka, Misri ina maslahi kwamba mapigano katika ukanda wa Gaza baina ya makundi mawili ya Kipalastina, Hamas na fatah, yanakoma, na fikra za kansela huyo wa Ujerumani na zile za mkuu wa Misri yaonesha zinafanana. Wote wnatambua fika kwamba mzozo baina ya Wapalastina na Wa-Israeli hauwezi kutanzuliwa kwa mwezi au mwaka mmoja. Mwenyewe Husni Mubarak kwa miaka 26 amekuwa akiushughulikia mzozo huo na kila wakati amekuwa akipigiana simu na Rais Mahmud Abbas wa Palastina. Mzozo baina ya Wa-Israeli na Wapalastina hivi sasa umegeuka kuwa ni moja ya mizozo kadhaa katika Mashariki ya Kati na umewapa motisha Waislamu wenye siasa kali kuzidi kuleta michafuko. Jambo hilo limetambuliwa na wadau wote wanaoushughulikia mzozo huo, lakini hawakubaliani suluhisho liwe la aina gani.

Katika ziara yake ya Mashariki ya Kati, Kansela Merkel, amefuatana pia na wanasiasa wa vyama vya upinzani vya hapa Ujerumani. Marieluise Beck wa Chama cha Kijani, alsema hivi juuya mchango wa nchi za Kiarabu katika mzozo wa Mashariki ya Kati.

+ Umoja wa Nchi za Kiarabu, Arab League, hasa Misri na saudi Arabia, hivi sasa sasa zinafanya mazungumzo ya kina na wawakilishi wa vyama vya Hamas na fatah kwa matumaini kwamba wataletwa pamoja ili waunde serekali ya Umoja wa Taifa. Kwani ni wakati sasa kujazwa pengo hilo la kutokuweko taasisi yenye mamlaka ambayo mtu anaweza kufanya nayo mashauriano. Lazima mambo yasonge mbele. Hilo ndilo suala kubwa. Ndoto ya fikra yetu ya kisiasa ni kupata mwanya.+

Wamarekani, kutokana na hali ngumu sana wanayokabiliana nayo huko Iraq na nchi za Kiarabu zenye siasa za wastani zikihofia juu ya kupanuka ushawsihi wa Iran katika eneo la Ghuba ni mambo yaliofanya kujongeleana baina ya Wapalastina na Wa-Israeli kuwe kugumu zaidi. Pia shambulio la kigaidi lilofanywa wiki iliopita katika mji wa pwani wa Eilat huko Israel linaashiria kwamba wenye siasa kali katika upande wa Wapalastina wanahisi na kuzihofia harakati zilioko mbioni hivi sasa za kutaka kuupa uhai mpya mwenendo wa amani. Ni kawaida katika mzozo huu wa Wa-Israeli na Wapalastina kwamba kila pale dirisha la amani linapotaka kufunguliwa, basi kunatokea vitendo vya kuvuruga juhudi hizo. Lakini mara hii tamaa imezuka kwa vile, licha ya yote yaliotokea karibuni, serekali dhaifu ya Israel chini ya waziri mkuu Ehud Olmert imeashiria kwamba iko tayari kuwa na mdahala zaidi na Rais wa Wapalastina, Mahmud Abbas.

Haikataliki kwamba ni kutokana na juhudi za Kansela Angela Merkel ndio sasa zile pande nne zinazohusika na mzozo wa Mashariki ya Kati, Russia, Marekani, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya zimeamua kuupa uhai mwenendo huo wa amani wa Mashariki ya Kati. Alipokuwa njiani kuelekea Mashariki ya Kati, Kansela Angela Merkel alikuwa na haya ya kusema:

+Naamini Marekani iko tayari kubeba dhamana. Bila ya Marekani hakutaweza kuweko maendeleo. Jambo hilo ni wazi kwangu. Lakini Ulaya inatakiwa ibebe dhamana zaidi. Nami naamini kwamba tunaweza uzuri kuowanisha mambo pindi tukizitumia pande nne zinazohusika na mzozo huo. Pande hizo ni sehemu ya ramani ya amani na kwa hivyo nahisi pande hizo ni muhimu kuchangia. Wadau wa mzozo huu wachangie kuleta utulivu na lazima watiwe moyo. Jambo hilo sisi tunaweza kulifanya. Ikiwa lazima kuweko amani, basi lazima kila mmoja azibake harakati za kuleta amani hiyo. Jambo hilo linafanywa na waziri mkuu wa Israel na pia na rais wa utawala wa ndani wa Wapalastina, nasi tunataka kuwasaidia.+

Mengi yatategemea juu ya kuitishwa mkutano wa pande tatu- waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Bibi Condoleeza, waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmbert na Rais wqa Wapalastina, Mahmud Abbas. Masharti ya kimsingi ya kupatikana maendeleo yeyote ni Wapalastina kuitambuwa haki ya Israel kuishi kama nchi, na jambo hilo ndilo linalofanya hadi sasa isiwezekane kuingizwa serekali ya Wapalastina ya Chama cha Hamas katika mashauriano yeyote. Lakini Chama cha Hamas sio rahisi kukishinda, kijeshi, kama vile ilivyoshindikana kwa Chama cha Hizbullah kushindwa huko Lebanon. Hivyo ni muhimu kuwaoneshea Wapalastina faida wazi watakazozipata pindi mipaka itakapokuwa wazi na maisha ya kila siku yakirejea kuwa ya kawaida baina yao na Israel.

Haikataliki kwamba Iran inachangia katika mizozo ya Mashariki ya Kati, kule Iraq, Lebanon na katika maeneo ya Wapalastina. Sio siri kwamba Iran inayasaidia makundi fulani ya Iraq yanayotaka majeshi ya uvamizi ya Kimarekani yatoke nchi hiyo. Sio siri kwamba Chama cha Hizbullah cha Lebanon kinachotaka kuiondosha madarakni serekali ya waziri mkuu Fuad Siniora katika nchi hiyo pia kinapata msaada wa hali na mali kutoka Tehran, na pia sio siri kwamba Chama cha Hamas cha Wapalastina kimepata msaada wa mali kutoka watawala wa Iran. Kwa hivyo uhasama wa Marekani na Iran, hasa kuhusu hoja ya Iran ya kutaka kumiliki nishati ya kinyukliya, unaathiri kwa namna moja au nyingine masuala ya kupatikana usalama katika maeneo ya Mashariki ya Kati. Na unahamishiwa katika maeneeo hayo ya mizozo. Kansela Angela Merkel wa Ujerumani anafahamu mafungamano yalioko katika masuala hayo:

+Kitisho kinachotokana na mpango wa kinyukliya wa Iran kinachangia sana, nahisi. Naamini hali hiyo imepelekea kuweko uwiano zaidi juu ya mambo mengi. Hiyo ina maana kwamba wadau katika eneo hilo washirikiane zaidi. Lazima wasaidiwe na lazima jambo hilo liendelezwe.+

Umoja wa Ulaya, na Ujerumani ikiwa inaouongoza Umoja huo hivi sasa, unabidi, angalau, uchukuwe jukumu la dhati la kuwa dalali wa kweli katika eneo hilo la Mashariki ya Kati. Mwishowe kuna maslahi ambayo Ujeruman itayapata katika kufanya hivyo, na jambo hilo linaonekana na ule mfano wa operesheni ya kijeshi ya kuweka amani huko Libanon ambapo Ujerumani inachangia.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com