1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel ziarani kisiwani Cyprus

11 Januari 2011

Kiongozi wa serikali kuu ya Ujerumani asisitiza umuhimu wa kuona juhudi za kuleta amani zinafanikiwa na kuungana upya kisiwa kisiwa cha Cyprus. Mazungumzo kati ya pande zinazohasimiana yanaanza upya kesho.

https://p.dw.com/p/zwKI
Kansela Merkel na rais Christofias wa CyprusPicha: AP

Ziara hiyo ya masaa kadhaa imesifiwa na serikali na vyombo vya habari vya Cyprus kuwa ni ya "kihistoria" na yenye "umuhimu mkubwa kisiasa."

Zypern Karte
Ramani ya kisiwa cha CyprusPicha: AP

Gazeti la kikoministi linaloelemea upande wa serikali Haravgi liliandika kwa kijerumani kichwa cha maneno cha ukurasa wake wa kwanza-Willkommmen-(Karibuni) huku gazeti la mrengo wa kulia Simerini likizungumzia juu ya ziara fupi lakini muhimu.

Katika ziara hiyo ya masaa matano mjini Nicosia-ya kwanza kuwahi kufanywa na kiongozi wa serikali ya Ujerumani katika jamhuri ya Cyprus,kansela Angela Merkel amesifu moyo na juhudi za papo kwa papo za kuzungumza na upande wa kaskazini unaodhibitiwa na Uturuki."Mmedhihirisha nia ya kutaka kufikia maridhiano ambayo mpaka dakika hii kwa bahati mbaya bado haijajibiwa." amesema mwanasiasa huyo wa chama cha Christian Democratic baada ya mazungumzo pamoja na rais wa sehemu inayoelemea upande wa Ugiriki, Dimitris Christofias.

"Sisi nchini Ujerumani na mimi binafsi ,tunajua vilivyo nini tafsiri ya nchi iliyogawika." Amesisitiza na kuelezea matzumaini yake kuiona nchi hiyo ikiungana upya.

Ledra Strasse in Nikosia Zypern
Barabara-Ledra-inayotenganisha Cyprus ya kaskazini na kusiniPicha: AP

Rais Christofias amemshukuru kansela Merkel akisema Ujerumani ni mshirika muhimu wa Cyprus katika Umoja wa Ulaya.

Mbali na mazungumzo hayo kansela Angela Merkel alitembelea pia eneo lililotengwa na umoja wa mataifa,alisalia kwa muda katika taasisi ya Goethe na kuzungumza na mkuu wa tume ya Umoja huo kisiwani humo Lisa Buttenheim.

Ziara ya kansela Angela Merkel imesadifu siku moja kabla ya rais wa sehemu ya Cyprus inayoelemea upande wa Ugiriki Demetris Christofias kukutana na mkuu wa sehemu ya kisiwa hicho inayotambuliwa na Uturuki,Dervis Erogku ikiwa mara ya kwanza baada ya kusita kwa muda mrefu mazungumzo ya amani yaliyoanzishwa September mwaka 2008 na Umoja wa mataifa.

Kisiwa cha Cyprus kimegawika tangu mwaka 1974, kufuatia uvamizi wa sehemu ya kaskazini inashikiliwa na Uturuki -ikijibu mapinduzi yaliyoandaliwa na wazalendo wa Cyprus wenye asili ya Kigiriki,wakiungwa mkono na Athens na ambao lengo lao lilikuwa kukiunganisha kisiwa cha Cyprus na Ugiriki.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/dapd
Mpitiaji: Abdul-rahman